WANANCHI BUHINGU WAOKOLEWA NA ADHA YA USAFIRI

Na Mwandishi Wetu,  Kigoma.
Wananchi wa kata ya Buhingu Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma wanatatajia kuondokana  na adha ya usafiri baada ya serikali kupitia Hifadhi za Taifa TANAPA kutoa zaidi ya shilingi milioni 850 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara yenye kilomita 22 kwa kiwango cha changarawe itakayoanzia kata ya Buhingu hadi  Hifadhi ya Taifa ya Milima Mahale.

Sambamba na kurahisisha usafirishaji wa watalii kupitia kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara,  mradi huo unalenga kurahisha shughuli za kiuchumi kwa kusafirisha bidhaa pamoja na abiria ndani na nje ya hifadhi  na hata katika maeneo mengine ya mkoa wa Kigoma.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi mtendaji wa kijiji cha Buhingu Saidi Mkallah amesema, wamekuwa wakitumia masaa takribani nane  kwa nauli ya zaidi ya shilingi elfu 20 kufika Kigoma mjini kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao kwa kutumia usafiri  wa magari jambo ambalo linawagharimu  kwa kiasi kikubwa kwani kwa safari moja tu inawagharimu zaidi ya elfu 50,000/=.

“Kupunguza gharama za usafiri ilitupasa kutumia usafiri wa boti kwenda  mpaka Lukoma na kulala huko kwaajili  ya kupanda basi  kesho yake asubuhi kuelekea Kigoma mjini kwa nauli ya shilingi 25,000 " amesema Makala. 

Kwa upande wake mkuu wa hifadhi ya taifa Milima Mahale kamishna msaidizi uhifadhi Susuma Kusekwa amesema mradi huo pia  utachangia ongezeko la watalii wanaotumia barabara kwa kuwa awali hawakuwepo na watalii wengi kutokana na ukosefu wa miundombinu ya barabara inayofika  katika hifadhi.

Amesema awali watalii walikua  wanatumia usafiri wa anga na maji kupitia  ya MV  Liemba ambayo kwa sasa ipo katika matengenezo jambo ambalo liliongeza gharama za  usafiri na kupunguza idadi ya watalii katika hifadhi hiyo.

Sambamba na hilo Kasekwa amesema ujenzi wa barabara hiyo utasaidia jamii kupata barabara bora itakayosaidia kurahisha shughuli za usafiri ndani na nje ya hifadhi na hivyo kuimarika katika kipato chao.

Akizingumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo meneja TARURA Mkoa wa Kigoma Muhandisi Godwin Mpinzile amesema, serikali imetoa fedha hizo kwa lengo la kurahisisha niundomindu ya usafiri wa barabara.

"Barabara hii itakwenda mpaka hifadhi za Milima Mahale, watu wataweza kusafiri, wagonjwa wataweza kufika  hospital haraka, watu wanaweza kufanya shughuli zao za kimaendeleo, michikichi na samaki itaweza kufika sokoni kwa haraka kwa sababu ya barabara hii" alisema Mpinzile.

 Mpinzile ametoa wito kwa viongozi wa vijiji vya Mugambo, Buhingu, Nkonkwa, Katumbi na Kalilani vya Wilaya ya Uvinza kutoa elimu kwa wananchi watoe ushirikiano wakati wa kutelekeza mradi huo kwa kuwa kuna upanuzi wa pande mbili za barabara mita kwa mita 40

Post a Comment

0 Comments