ELIMU YA AWALI KUBORESHWA KUPITIA MRADI WA BOOST



Mwajabu Hoza , Kigoma 

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kigoma Mkoani Kigoma imepokea kiasi cha shilingi milioni 215.4  kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa ya elimu ya awali katika shule tatu kupitia mradi wa Boost ambao umelenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi.

Elimu ya awali ndio msingi wa elimu kwa wanafunzi wenye umri mdogo ambao wanaanza kuandikishwa shule ambapo serikali imeona ipo haja ya kuboresha mazingira kwa kuanza kutekeleza ujenzi wa madarasa na vyoo kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya awali.

 

Akizungumzia ujenzi huo Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Egzavery Ntambara amesema fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa miundombinu ya madarasa mawili , matundu ya vyoo mawili, madawati maalumu, mikeka pamoja na vifaa vya kuchezea.

 

“Ujenzi utafanyika katika shule tatu na kila shule itakuwa na madarasa mawili bora na vyoo viwili vya mfano ambapo gharama ya kila shule itakuwa ni shilingi milioni 71.8 ambayo itakamilisha ujenzi na vifaa muhimu vyote kwa ajili ya wanafunzi wa elimu awali kujifunzia” amesema.

 

Amesema wilaya hiyo inajumla ya shule za msingi 109 ambapo kati ya hizo shule tatu ndio zinatekeleza ujenzi wa madarasa ya awali ya mfano pamoja na matundu ya vyoo kwa wanafunzi wa elimu ya awali.

 

Amesema mradi wa Boost wa mwaka 2023 unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano na kila mwaka ujenzi wa vyumba vya madarasa utakuwa ukifanyika kwa shule hizo za msingi na kuhakikisha shule zote zinakuwa na madarasa ya awali.

 

Baadhi ya wananchi akiwemo George Kasendeli na Emmanuel Bahindu wakazi wa kijiji cha Kabale wanaishukuru serikali kwa kuwaletea mradi huo wa boost katika kijiji chao.

 

Wamesema watoto wao kwa sasa wanasoma katika mazingira hatarishi ambapo kukamilika kwa madarasa hayo kutasaidia kuondoa changamoto kwa wanafunzi ambao wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata shule lakini pia  msongamano mkubwa wa wanafunzi katika darasa moja.

 

Agatha Rusimbi anasema kwa sasa wanafunzi wanaoandikishwa shule wanakuwa na umri mdogo na wanalazimika kupita maeneo ya vichakani kuelekea shule jambo ambalo ni hatari sana kwa usalama wao hasa wale wa kike.

 

“Ujenzi wa shule hii katika eneo letu utatupunguza hofu ambayo tunayo juu ya watoto wetu ambao hadi sasa wanapita katika vichaka lakini pia changamoto za barabarani wakati wakivuka kuelekea shule iliyopo kijiji cha jirani hivyo kukamilika kwa shule hii itakuwa na manufaa makubwa sana kwetu na usalama wa watoto wetu utakuwa wa kutosha” amesema Agatha

 

Diwani kata ya Kalinzi Ignas Helanya anasema kata yake imepata ujenzi wa shule mbili za msingi ambapo shule ya msingi Amani itajengwa katika kijiji cha Kabale na shule ya msingi Bugugo ujenzi wake utakuwa katika kijiji cha Matyazo wilaya ya Kigoma.

 

Anasema ujenzi wa shule hizo utasaidia kupunguza changamoto mbalimbali ikiwemo idadi kubwa ya wanafunzi kwa baadhi ya shule pamoja na kuondoa changamoto ya utoro wa wanafunzi ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata shule.

 

Mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli amesema serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya elimu katika ujenzi wa miundombinu ya majengo, matundu ya vyoo na madawati na hivyo kupunguza mzigo mkubwa kwa wananchi ambao awali walilazimika kuchangia ujenzi huo na ununuzi wa madawati.

 

“Kwa sasa elimu ni bure kuanzia shule ya awali hadi kidato cha sita hivyo kazi yenu kubwa wananchi wangu ni kuangalia mahitaji muhimu ya watoto ikiwemo sare za shule , madaftari na kufuatilia kama anaenda shule,  hakikisheni kunakuwa na mawasiliano kati yenu na walimu kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni” amesema

 

Serikali imeendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kuongeza fursa za ujifunzaji wa awali ambapo kwa mwaka 2022/ 2023 kwenye mpango jumuishi wa Taifa wa makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto PJT – MMMAM  zaidi ya shilingi bilioni 109 zimetengwa kwa ajili ya uboreshaji huo.

 


Post a Comment

0 Comments