MKUU WA MKOA KIGOMA APIGA MARUFUKU UKUSANYAJI WA MAPATO NJE YA MFUMO WA TAUSI

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amepiga marufuku Halmashauri zote mkoani Kigoma kutumia mifumo tofauti na ule wa TAUSI katika kufanya makusanyo ya ndani kwenye Halmashauri hizo.

Andengenye ametoa Maelekezo hayo Juni 6, 2023 wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Madiwani Manispaa ya Kigoma/Ujiji kujadili Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha unaoishia Juni 30, 2022.

Mkuu wa Mkoa amesema kitendo cha kutumia mifumo ya zamani ya ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ikiwa ni pamoja na matumizi ya Risiti unaendelea kutoa mianya ya kufanyika kwa urasimu kwa baadhi ya watendaji wasio waaminifu.

‘’Kupitia Baraza hili ninatoa Maagizo kuwa ni marufuku kwa watendaji katika Halmashauri zote mkoani hapa kutumia au kuidhinisha matumizi ya mifumo tofauti na huu uliorasimishwa na Serikali katika kukusanya mapato ya ndani na watakao kaidi na kufanya kinyume watakuwa wanakiuka Maelekezo ya Serikali kwa makusudi na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao’’ amesisitiza.

Aidha kiongozi huyo amewataka Madiwani katika Halmashauri zote mkoani hapa kuzingatia kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma katika utendaji kazi wao.

‘’Epukeni matumizi mabaya ya Madaraka kupitia nafasi zenu, hii itawasaidia wananchi kuamini maamuzi mnayoyafanya na kuepuka malalamiko yasiyo na msingi katika jamii mnayoiongoza’’ ameshauri Andengenye.

Naye Meya wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Baraka Lupoli amesema upungufu wa watumishi katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji unachangia kwa kiasi kikubwa kupotea kwa mapato ya ndani hali inayosababaisha makusanyo kuwa chini ya kiwango.

‘’Makadirio ya makusanyo yetu kwa Mwezi ni zaidi ya Shilingi Mil. 400 ila kutokana na changamoto hizo, makusanyo yetu hushuka hadi kufikia kiasi cha Shilingi Mil. 270 kwa Mwezi’’ amesisitiza Mhe. Baraka.

Kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji imepata Hati Safi ya ukaguzi wa Hesabu za Serikali.

Post a Comment

0 Comments