SERIKALI KUFANYIA KAZI CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI SEKTA YA UFUGAJI NYUKI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto zinazoikabili sekta ya ufugaji nyuki lengo likiwa ni kuongeza hamasa ya wadau wengi kuingia katika sekta hiyo ili kufungua fursa ya ajira kwa vijana pamoja na kusaidia kuleta fedha za kigeni.

Hayo yamesemwa na Afisa Ufugaji Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na utalii wa Dawati la Sera pamoja na Sheria, Filipo Mwampamba wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo Juni 7, 2023 Jijini Dodoma mara baada ya kufanyika kwa mkutano wa wadau wa nyuki wa siku mbili uliozikutanisha sekta za Umma na Binafsi.

Amesema miongoni mwa mambo ambayo wadau wameiomba Serikali ifanyie kazi ni pamoja na changamoto ya uwepo wa tozo nyingi wakati wa kupeleka mazao ya nyuki nje ya nchi , pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kuchakatia mazao hayo.

“ Katika mkutano huu Wadau wamebainisha changamoto ya uwepo wa maeneo yanayofaa kwa ajili ya kuchakatia mazao pamoja na upatikanaji wa vifungashio ambavyo ukiangalia changamoto hizo tayari tumeanza kuzifanyia kazi.” amesema.

Ameongeza kuwa Mkutano huo umetoa fursa kwa Wadau hao kuwasilisha changamoto zao wanazokumbana nazo pamoja na kutoa mapendekezo ya namna ya kushughulikia changamoto hizo ikiwa mkutano wa kimkakati chini ya ufadhili wa Mradi wa Umoja wa Ulaya ujulikanao kwa jina la BEVAC 

“ Sisi kama Serikali tupo hapa kwa lengo la kusikiliza lakini pia kupokea ushauri na kisha kufanyia kazi kwa karibu ili kuchagiza uwekezaji katika ufugaji nyuki, Tunaishukuru Serikali ya Umoja wa Ulaya kwa kuwezesha vikao hivi muhimu.” ameongeza.

Kwa upande wa Linus Gedi Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na Maendeleo ya Sekta ya Ufugaji nyuki, amesema kupitia mkutano huo umekuwa muhimu sana kwao kwa vile wamepata fursa kuzungumzia vikwazo wanavyopitia wauzaji wa bidhaa za nyuki ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

“ Kuna taratibu ndefu sana ambazo wauzaji wa mazao ya nyuki wanapitia mpaka mzigo wake uingie kwenye meli na kwenda kwenye masoko, Tunataka Serikali itupunguzie huu mchakato ili biashara hii iwe na tija.” amesema.

Post a Comment

0 Comments