WAZAZI NA WALEZI KIGOMA/UJIJI ZUNGUMZENI NA WATOTO

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Wazazi na Walezi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji wametakiwa kuzungumza na Watoto wao kwa kuwapatia elimu ya kupinga vitendo vya ukatili pamoja na utoaji taarifa ili hatua za kisheria kuchukuliwa.

Nasaha hizo zimetolewa Leo June 15, 2023 na Mkuu wa dawati la jinsia na Watoto Mkoani Kigoma Inspecta Maiko Mjema katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Manispaa ya Kigoma Ujiji katika viwanja wa shule ya Sekondari Katubuka.

Katika Maadhimisho hayo amewataka Wazazi, Walezi na Jamii kwa ujumla kuwalinda watoto kwa kuwaepusha na maeneo hatarishi yanayoweza kuchochea vitendo vya ukatili.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi, Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii, Ndugu Deodatus Nenze amesema serikali itaendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali ili kuendelea kutokomeza vitendo vya ukatili kwa kuzingatia Sera, Miongozo na kanuni zinazotoa haki kwa Watoto.

Ameongeza kuwa Halmashauri imepanga kufanya Shindano la kuibua vipaji vya watoto ili kuhakikisha malengo yao yanafikiwa.       

Ameendelea kusema tayari mabaraza ya kushughulikia Masuala ya watoto tayari yameundwa kwa kata zote kumi na tisa na mitaa Sitini na nane,  na Uanzishaji kituo cha huduma ya watoto (One stop centre) Hospitali ya Rufaa Mkoani Kigoma Maweni.

Maadhimisho ya mtoto wa Afrika hufanyika June 16, kila mwaka na kwa mwaka huu yamehusisha Michezo ya kucheza mziki, Uvutaji Kamba, Maigizo na kukimbiza Kuku huku yakienda na kauli Mbiu isemayo "Zingatia usalama wa Mtoto katika ulimwengu wa Kidigitali"


Post a Comment

0 Comments