DKT. MSONDE AAGIZA KASI YA UJENZI MIUNDOMBINU YA KIDATO CHA TANO KUONGEZWA

Na Mwandishi Wetu, Singida
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu), Dkt. Charles Msonde amezitaka Halamashauri zote zilizopokea fedha kwa ajili ya Ujenzi wa Miundombinu ya Upanuzi wa shule za sekondari kwa Kidato cha tano na sita kuongeza usimamizi na kasi ya ujenzi na kuhakikisha miundombinu yote inakamilika ifikapo tarehe 30 Julai 2023.

Ameeleza hayo leo tarehe 09 Julai 2023 katika mwendelezo wa ziara yake katika Halmashauri za wilaya ya Manyoni, Itigi, Ikungi na Halmashauri ya wilaya Singida kukagua ujenzi wa miundombinu hiyo inayoendelea kutekelezwa.

“Kazi za ujenzi zinaendelea vizuri lakini changamoto iliyopo ni kasi ya ujenzi haitoshi kutokana na mafundi kuwa wachache katika maeneo mengi ambayo madarasa na mabweni na miundombinu mingine inaendelea kujengwa” amesema Dkt. Msonde

Dkt. Msonde amewataka kuongeza nguvu kazi ya Mafundi ili kufanya kazi kubwa kwa muda mfupi ikiwa ni pamoja na kufanya kazi usiku na mchana na kuhakikisha miundombinu inakamilika bila kuathiri Ubora na viwango vya kitaalam.

“Bado tumebakiza siku 20 tu za kukamilisha miundombinu hii, kwahiyo tunaweza kusahihisha mapungufu yaliyopo na kuhakikisha ifikapo  tarehe 30 Julai 2023 tunakamilisha ili tarehe 13 Agosti 2023 wanafunzi wanaokuja kuendelea na masomo waweze kutumia mabweni na madarasa haya”

Dkt. Msonde amesema Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kujenga Vyumba vya madarasa, Mabweni na Miundombinu mingine nchi nzima ili kuhakikisha wanafunzi wote wa Kidato cha tano wanaendelea na masomo katika mazingira mazuri ya kujifunza.
 
Aidha, Dkt. Msonde amesisiza kufuatwa kwa miongozo iliyotolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI katika ujenzi wa miundombinu hiyo.

Post a Comment

0 Comments