HUDUMA BORA ZIENDANE NA UWEKEZAJI ULIOFANYIKA - DKT. MAHERA

Na. Mwandishi Wetu, Mbozi - Songwe
Serikali imewataka Waganga  Wafawidhi wote nchini  kuboresha utendaji kazi ili kuweza kuendana na thamani ya uwekezaji uliyofanyika kwenye  vituo vya kutolea huduma.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt Charles Mahera wakati wa ziara yake ya kikazi ya  kutembelea Kituo cha Afya cha Isansa na Hospitali ya Wilaya ya Mbozi –Vwawa Mkoani Songwe.

Dkt. Mahera amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa pesa nyingi katika kuboresha sekta ya afya nchini ambapo maboresho hayo ni ujenzi wa majengo mapya, ukarabati wa vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba na dawa.

“Tukifanya kazi kwa kufuata miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya, weledi, maadili na ushirikiano  kwa kuzingatia muda wananchi wataweza kupata huduma bora za afya kutoka ngazi ya msingi  itakayo kuwa sambamba na uwekezaji uliofanywa na serikali yao" ameeleza Dkt. Mahera

Dkt. Mahera ameongeza kuwa watumishi wa Afya wanatakiwa kuzingatia miongozo ya huduma ya  afya pamoja na kujali muda wa kazi ili kuleta ufanisi katika kutoa huduma bora 

Ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuangalia maendeleo ya vituo vya huduma za afya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ambao ndio watunga sera ili kuboresha huduma bora kwa wananchi.

“Naomba watumishi wa Afya muendelee kujituma katika kuwahudumia wananchi kwani serikali iko bega kwa bega na nyinyi katika kuboresha maslahi yenu ili kuwa na mazingira mazuri ya kazi”, amesema  Dkt. Mahera.

Aidha amemuelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Boniface Kasululu kuhakikisha anashirikiana  na Timu za usimamizi na uendeshaji wa huduma za Afya ngazi ya Mkoa na Halmashauri (RHMT na CHMT)  kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa dawa, vifaa tiba na huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma ili kuleta ufanisi wa kazi na kupata takwimu sahihi za mahitaji kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe ametoa wito kwa watumishi wa afya nchini kutofanya kazi kwa kwa mazoea bali kufuata taratibu za kazi

Post a Comment

0 Comments