JAMII KIGOMA IMETAKIWA KUWAENZI MASHUJAA KWA KUPIGA VITA UJINGA UMASIKINI NA MARADHI


Na Mwandishi Wetu, Kigoma

Jamii mkoani Kigoma imetakiwa kuwaenzi Mashujaa na waasisi wa Taifa la Tanzania kwa kuendelea kupambana dhidi ya Ujinga, Maradhi na Umasikini ili kujiletea Maendeleo. 

Akizungumza mara baada ya kuongoza Zoezi la Usafi wa Mazingira katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma Maweni ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa nchini, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema kila mtu anawajibu wa kuchukua hatua Madhubuti katika kukabiliana na kasi ya Maendeleo duniani.

Amesema Jamii inapaswa kujikinga na  maradhi ili kunusuru  fedha  zilizotengwa na serikali kwa ajili ya kugharamia  matibabu na kuzielekeza  katika utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo. 

Aidha Andengenye ameitaka jamii kukabiliana na ujinga kwa kuhakikisha watoto wanapata elimu itakayowasaidia kuendana na mabadiliko katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo duniani. 

Amesisitiza kuwa, kila mtu anapaswa kujibiidisha  na kujituma katika kufanya kazi  na kujikomboa  dhidi ya  hali ya umasikini. 

"Vita tunayopigana sasa hatuhitaji silaha bali ni za kifikra kwa lengo la kujikomboa  dhidi ya  Maadui Ujinga, Umasikini na Maradhi" amesema Andengenye. 

Katika hatua nyingine Kiongozi huyo ameziagiza Halmashauri zote mkoani Kigoma kuhakikisha zinaendelea  kutekeleza agizo la serikali la kutenga  siku moja kila mwezi kwa ajili ya kufanya zoezi la usafi wa mazingira. 

Ameongeza kuwa lengo la kutekeleza agizo hilo  ni kuiepusha jamii dhidi ya maradhi yanayozuilika na kujenga utamaduni wa uwajibikaji binafsi katika kutunza Mazingira.

Post a Comment

0 Comments