KAMPUNI YA ORYX YAWAKUMBUKA WAJAWAZITO WILAYA YA BUHIGWE

Na Editha Karlo, Kigoma.
KAMPUNI ya oryx energies imekabidhi mitungi ya gesi 300 ya kupikia yenye kilo 45 kwa wanawake wajawazito Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma ikiwa ni kama hatua za kuhakikisha mama mjamzito analea vizuri ujauzito wake ikiwa ni sambamba na kutunza mazingira kwa kutokata miti ovyo.

Akizungumza kabla ya kukabidhi mitungi hiyo ya gesi kwa wajawazito katika hospital ya Wilaya ya Buhigwe wakati akipokea misaada mbalimbali kutoka Taasisi ya Doris Mollel Foundation na Tume ya ushindani ya haki(FCC) Makamu wa Rais Dkt Philipo Mpango ameipongeza kampuni ya oryx kwa kutoa mitungi hiyo na kusema kuwa hiyo inaonyesha jinsi gani wanavyomthamini mama mjamzito na kiumbe chake alichonacho tumboni.

Dkt. Mpango amesema, serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu imekuwa ikifanya maboresho makubwa katika sekta ya afya, hususani afya ya mama na mtoto ikiwemo afya ya  mtoto njiti.

“Niipongeze Taasisi ya Doris Foundation pamoja na taasisi zingine walizoshirikiana kwa mchango wao wa kusaidia jamii ya watoto njiti pamoja na kufanikiwa kuleta vifaa tiba kwaajili ya watoto njiti katika Wilaya ya Buhigwe”amesema Dkt Mpango.

Awali Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation ameeleza sababu ya kuomba mitungi hiyo ya gesi ya kupikia kwa ajili ya kinamama wajawazito kwa kuwa anatambua changamoto wanazokumbana nazo hivyo ni vyema wakaachana na kutumia kuni badala yake watumie majiko ya gesi kwaajili ya usalama wao pamoja na mtoto aliyetumboni.

Nae Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Oryx  Alex Wambi ambaye ni meneja mauzo kanda ya kaskazini amesema kuwa, wameamua kutoa mitungi hiyo ya gesi kama zawadi kwa akina mama wajawazito kwasababu wanajua changamoto wanazopita akina mama hao katika kipindi hicho.

“Kipindi mama anakuwa mjamzito huwa anakutana na changamoto nyingi kama asipozidhibiti mapema zinaweza kumletea matatizo na kupelekea kujifungua mtoto ambaye hajatimiza umri (njiti) ndiyo maana tumewapa hawa akina mama haya majiko ya gesi pamoja na elimu ya jinsi ya kuyatumia vizuri”amesema.

Naye mmoja wa akina mama wajawazito aliyepata jiko la gesi na mtungi wake aliishukuru kampuni ya oryx kwa kuwapatia majiko hayo pamoja na kuwasadia katika kulinda afya zao na watoto pia itasaidia kutunza mazingira.

“Tunaipongeza serikali na oryx kwa msaada waliotupa wa haya majiko ya gesi,tunaomba wahusika wa waliotupa hii mitungi ya gesi waangalie namna ambayo tutaweza kuipata kwa bei nafuu huku vijijini bei ambayo tutaweza kuzimudu”alisema


Post a Comment

0 Comments