MAKAMU WA RAIS AWATAKA WANANCHI KUTUMIA FURSA YA KUWEKEZA NCHINI

Na Editha Karlo,Kasulu Kigoma
MAKAMU wa Rais, Dkt Philip Mpango amewataka watanzania kutumia fursa ya kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ili kuweza kukuza uchumi wa mtu mmoja na Taifa kwa ujumla.

Dk Mpango ameyasema hayo leo Wilayani Kasulu mkoani Kigoma wakati akifungua Hotel ya Bwami Dubai iliyojengwa na mwekezaji mzawa wilayani humo na kusema serikali imeweka mazingira rafiki ya uwekezaji ikiwa ni sambamba na kuanzisha miradi ambayo wananchi watanufaika nayo.

Ameongeza kwa kusema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Hassan Suluhu imeondoa tozo na kodi mbalimbali ambazo zilikuwa ni kero kwa wafanyabiashara na wawekezaji.

“Sasa hivi sekta binafsi ndo zimekuwa zikitoa ajira kwa wingi,kama hapa kwenye hii hotel najua ajira nyingi watapata wazawa wa hapa Kasulu hivyo kuchochea uchumi wa Wilaya hii kukua” amesema.

Naye Mkurugenzi wa hotel ya Bwami Dubai, Evance Chocha ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hali iliyofanya kujenga hotel hiyo ya kisasa katikati ya mji wa Kasulu.

“Hotel hii imegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.6 hadi kukamilika ujenzi wake, na inajumla ya vyumba 36 na chumba cha bei ya chini kikiwa ni shilingi elf 60 huku chumba cha bei ya juu kikiwa shilingi laki moja na elf ishirini pia kuna ukumbi wa mkutano wenye uwezo wa kuchukua watu 50 kwa wakati mmoja”amesema

Mmiliki wa hotel hiyo amesema kuwa kwenye uwekezaji huo aliofanya ameweza kutoa ajira 45 kwa watanzania ambao asilimia kubwa ni wazawa wa Kasulu.

“Hotel hii itachangia kukuza uchumi katika Wilaya ya Kasulu na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla kwani manunuzi mbalimbali yatafanyika, wageni kutoka maeneo mbalimbali watafika hapana kuongeza mzunguko wa fedha” ameongeza.

Post a Comment

0 Comments