MAKAMU WA RAIS AWATAKA WANAUME KUACHA TABIA YA KUPIGA WANAWAKE WAJAWAZITO.

Na Editha Karlo,Kigoma
MAKAMU wa Rais  wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewataka wanaume wenye tabia za kupiga wake zao wakati wakiwa wajawazito kuacha mara moja tabia hiyo kwani imechangia kuwapa akina mama wajawazito msongo wa mawazo na  kupelekea kuzaliwa kwa watoto kabla ya wakati (watoto njiti).
 
Dk.Mpango ameyasema hayo leo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma  kwenye hospital ya Wilaya hiyo alipokuwa akipokea misaada mbalimbali iliyotolewa na taasisi ya Doris Mollel Foundation na Tume ya ushindi wa haki (FCC) kwa ajili ya kusaidia kukabili changamoto ya watoto njiti kwenye hospitali ya wilaya Buhigwe.

“Kwakweli tabia hii haikubaliki hata kidogo  kwani pamoja na athari ya kiafya kwa wanawake wajawazito wanaopigwa lakini imesababisha msongo wa mawazo kwa wanawake hao hivyo kuzaa watoto ambao hawajatimiza umri wa kuzaliwa na kufanya ongezeko la watoto njiti linazidi kuwa kubwa badala ya kupungua”amesema

Dkt Mpango amempongeza Doris Mollel kwa kitendo cha kuanzisha taasisi  ya kusaidia kupunguza changamoto ya watoto njiti na kuongeza kuwa taasisi yake inatakiwa kuungwa mkono na wadau wote wa serikali na hata ambao siyo wa serikali.

Aidha Dkt Mpango amewapongeza mwanamziki Ally Kiba na Mbwana Samatta kupitia taasisi yao ya SAMAKIBA kwa kuchangia fedha za kununua vifaa kwaajili ya watoto njiti ambapo walicheza mechi ya hisani na pesa zilizopatikana zimesaidia kununua vifaa hivo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi toka Tume ya ushindani wa haki(FCC) kwa niaba ya Mkurugenzi mkuu wa tume hiyo Monica Mosha wakati akikabidhi vifaa kwa Halmashauri ya wilaya Buhigwe, amesema kuwa tume hiyo imekabidhi vifaa tiba kwa ajili ya sekta ya afya kwenye vituo vya afya vilivyopo pembeni ya wilaya ya Buhigwe hususani vya kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi.
 
Moshi ametaja vifaa vilivyokabidhiwa kuwa ni Mashine 16 za kupima shinikizo la damu, vitanda saba vya kujifungulia wajawazito, vitanda viwili vya kupimia wagonjwa na vitanda vitatu vya kulalia wagonjwa, sanction mashine moja, magodoro 17 ya kulalia wagonjwa, mashuka 10, mashine mbili za kupima oksijeni, darubini moja na mashine 11 za kupima wingi wa damu.

Sambamba na hilo Mkurugenzi huyo amesema kuwa FCC imekabidhi mashine tano za kupima mapigo ya moyo wakati mtoto akiwa tumboni.

Nae Doris Mollel Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation amesema kuwa taasisi yake imekuwa ikisimamia na kuendesha taratibu ya kusaidia watoto njiti kutokana na changamoto kubwa inayowakabili wajawazito wanaoijifungua watoto hao na kufanya ukuaji na malezi yao kuwa na mashaka.

“Taasisi yetu hii ya Doris Mollel Foundation ina miaka 8 toka ianzishwe tumeshatoa misaada kwenye vituo 63 nchi na hapa leo ni kituo cha 64 nina hamasika kufanya hivi sababu hata mimi nilizaliwa tukiwa mapacha ila tulizaliwa hatujatimiza umri(njiti) kwahiyo changamoto za watoto njiti nimezipitia pia”amesema Doris

Doris Mollel Foundation wamekabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 190 ikiwa ni sehemu ya kiasi cha shilingi bilioni 1.3 ambazo taasisi hiyo imetumia kwa ajili ya misaada ya mpango wa kusaidia watoto njiti toka ilipoanzishwa mwaka 2015.


Post a Comment

0 Comments