MAMA AMCHOMA MOTO MKONONI MTOTO WAKE AKIMTUHUMU KUIBA MUWA

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina la Esther Damiani mwenye umri wa miaka 30 mkazi wa kitongoji cha Uwanjani kata ya Mwandiga halmashauri ya wilaya ya Kigoma amemchoma mikono mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka mitano kwa kutumia moto wa mkaa akimtuhumu kuiba muwa.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Tito Mahamudu Kilalika Mwenyekiti wa kitongoji cha Uwanjani kata ya Mwandiga amesema baada ya kupewa taarifa walifika nyumbani kwa mwanamke huyo na kumpeleka mtoto huyo kupata huduma ya kwanza huku taratibu za kumfikisha katika vyombo vya sheria mwanamke yule zikiwa zinaendelea.

Naye Esther Damiani, mama mzazi wa mtoto huyo amesema makosa mengi aliyoyafanya mtoto wake ndiyo sababu iliyopelekea kumchoma mikono ili asiendelee na tabia ya wizi.

Akizungumzia sakata hilo Katibu wa Dawati la Jinsia katika kijiji cha Mwandiga Halmashauri ya Wilaya Kigoma Zuhura Kassimu Kasheshe amesema mtoto anapofanyiwa vitendo hivyo vya ukatili inampelekea kupata tatizo la kisaiklojia.

Nao baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo akiwemo Pius Paul wamesema vitendo hivyo sio vizuri kwani vinamfanya mtoto ashindwe kujiamini kutokana na wengi wao kufanyiwa vitendo vya ukatilii wa aina hiyo.

Post a Comment

0 Comments