MATAWI YA BENKI SASA KUFIKA KIJIJI KWA KIJIJI NCHINI.

Na Isaac Aron, Kigoma
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, ametoa wito kwa taasisi za kifedha, hususan mabenki, kusogeza matawi yao katika maeneo ya vijijini ili kufikisha huduma za kifedha karibu na wananchi. 

Dkt. Mpango amebainisha kuwa wananchi wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo, na wengine wamelazimika kuhifadhi fedha zao nyumbani ambapo usalama wa fedha hizo ni mdogo.
 
Ametoa agizo hilo wakati alipokuwa akifungua tawi jipya la Benki ya Taifa ya Biashara (NMB) katika wilaya ya Buhigwe, mkoani Kigoma ambapo tawi hilo ni la sita katika mkoa huo na la 229 nchini kote.

Wilaya ya Buhigwe, iliyoko mkoani Kigoma, inakabiliwa na changamoto kubwa ya huduma za kifedha ambapo baadhi ya wananchi kutoka vijiji mbalimbali wamekuwa wakilazimika kutembea umbali wa takribani kilometa 140 kwenda na kurudi wilaya ya Kasulu ili kupata huduma za kifedha katika benki wanapohitaji.
 
Dkt. Philip Mpango amewaomba taasisi za kifedha kuchukua hatua na kuanza kuangalia uwezekano wa kufungua matawi katika maeneo hayo ambapo wananchi wamekuwa hawana uhakika na usalama wa fedha zao.
 
Kwa upande wao Wakazi wa wilaya ya Buhigwe wamezungumza na Blog hii kueleza changamoto wanazokabiliana nazo kutokana na ukosefu wa tawi la benki katika eneo hilo ambapo Frank Remy na Samalati Abdalah, wakazi wa Buhigwe, wametoa ushuhuda wa jinsi wanavyopata taabu kutafuta huduma za kifedha.
 
Benki ya NMB imefungua tawi lake la kwanza katika wilaya ya Buhigwe na inatarajiwa kutoa mikopo yenye thamani ya takribani shilingi bilioni moja kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa eneo hilo. 

Nae Filbert Mponzi, Afisa Mkuu wa Wateja na Biashara wa NMB, pamoja na Dkt. Edwin Mhede, Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, wamezungumza juu ya fursa hii mpya na jinsi itakavyochangia katika maendeleo ya wilaya ya Buhigwe.
 
Katika hatua nyingine, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa taasisi za kifedha kupunguza gharama za huduma za kifedha mtandaoni ili kuwavutia wananchi wengi zaidi kutumia huduma hizo ambapo Hatua hii itasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kuwawezesha wananchi kufanya miamala kwa urahisi.
 
Uzinduzi wa tawi la Benki ya NMB katika wilaya ya Buhigwe umekwenda sambamba na utoaji wa misaada ya vitanda kwa shule na vituo vya afya ikiwa ni vitanda vya akina mama kujifungulia, pamoja na mabati vyenye thamani ya shilingi milioni 82.4 hatua ambayo inaonyesha dhamira ya benki hiyo kusaidia jamii na kuchangia katika maendeleo ya eneo hilo.

Post a Comment

0 Comments