MKANDARASI APEWA SIKU 15 KUJITAFAKARI

Na Isaac Aron, Kigoma
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Mkame Mbarawa, ametoa notisi ya siku 15 kwa mkandarasi Sinohydro Corporation, anayejenga kipande cha pili cha barabara ya Kabingo Mnyovu Mkoani Kigoma, kufikisha mitambo eneo la kazi ili kukamilisha mradi huo kwa wakati. 

Mkandarasi huyo ambaye anajenga kipande cha Kanyani Mvugwe chenye urefu wa kilometa 70.5 kwa gharama ya shilingi bilioni 83.7, hadi sasa amefikia asilimia 65.30, huku akibakiwa na muda wa miezi miwili na nusu kwa mujibu wa mkataba.

Kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Kabingo Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.1 unatazamiwa kuwa alama kubwa kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma, ambao wamekuwa wakisubiri ufunguzi wa barabara hiyo kwa muda mrefu.

Hata hivyo, matumaini hayo yameanza kuingia dosari kutokana na baadhi ya wakandarasi kushindwa kufuata kasi inayotakiwa katika utekelezaji wa kazi, hali ambayo imemfanya Waziri Mbarawa kutoa kauli ya Serikali baada ya kutembelea mradi huo.

Aidha Waziri Mbarawa amewataka Wakala wa barabara nchini TANROADS kufanya ukaguzi katika miradi inayotekelezwa ili kubaini changamoto na kuzitatua kwa lengo la kuondoa sintofahamu.

Wakandarasi wengine watatu wanaotekeleza mradi huo wameripotiwa kufanya vizuri, na baadhi ya maeneo ya barabara tayari yamekamilika na kuanza kutumika, hivyo kuwaletea wananchi faida.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo Manyovu unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 360.5, unatakiwa kukamilika mwaka huu kwa vipande vyote vinne.

Hata hivyo, muda uliobaki unahitaji mkandarasi kufanya juhudi za ziada ili kukamilisha kazi kwa wakati uliopangwa na kuleta manufaa kwa jamii ya Kigoma.

Post a Comment

0 Comments