MWONGOZO WA UOMBAJI MIKOPO 2023/24 WAZINDULIWA

Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omar Kipanga amesema Elimu ni nyenzo muhimu sana katika Maendeleo, kwa kutambua hilo serikali ipo kwenye hatua mbalimbali za mageuzi, ikiwa ni pamoja na kuimarisha  mfumo wa Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Mhe. Kipanga ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam Julai 13, 2023 akizindua rasmi Mwongozo wa uombaji Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka 2023/2024.

Mwongozo huo unaelekeza  maombi kufanyika kwa njia ya mtandao na dirisha litakuwa wazi kuanzia Julai 15 mpaka Oktoba 15, 2023.

Mhe. Kipanga ameongeza kuwa ingawa Mwongozo huo utapatikana kuanzia leo, Wanafunzi, wazazi na walezi watapaswa kutumia siku hizi mbili kuusoma na kuuzingatia kabla ya kuanza kuomba.

"Katika Mwongozo huo waombaji mkopo hawata tuma nakala ngumu wala kuja Bodi ya Mikopo badala yake watatuma nakala laini, hii ni kutokana na maboresho makubwa ya mfumo wa uombaji yaliyofanywa kupitia ufadhili wa Mradi wa Elimu ya Juu Kwa mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ." alisema Mhe. Kipanga

Aidha ili kurahisisha zoezi la malipo Mhe. Kipanga amesema Mwongozo unamtaka muombaji Kufungua akaunti ya SIPA (Student's Individual Permanent Account) kwa ajili ya kufuatilia maombi yake ya mkopo, kuwa na Akaunti ya Benki aipendayo pamoja na nambari ya simu iliyosajiliwa.

Pia amewakumbusha kwamba Mwongozo huu hautawahusu waombaji katika ngazi ya Stashahada, kwani taratibu zinaandaliwa na Mwongozo utatolewa hivi karibuni.

Kipanga ameipongeza Bodi hiyo kuandaa maboresho ya mfumo na  Mwongozo huo na  huku akibainisha kuwa serikali katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita imeongeza bajeti ya fedha za Mikopo ya Elimu kutoka shilingi Bilioni 570 (2021-2022) hadi shilingi Bilioni 731 kwa mwaka huu mpya wa masomo utakaonza Oktoba, 2023.

"Ongezeko hili la fedha limewezesha idadi ya wanufaika wa Mikopo kuongezeka kutoka 177,615 mwaka 2021-2022 hadi wanufaika 205,000 kwa mwaka huu mpya wa masomo". amebainisha Mhe. Kipanga


Post a Comment

0 Comments