RAIS SAMIA ATAMANI KUONA JESHI LA KUJENGA TAIFA (JKT) LINAKUWA LA KISASA


Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Rais wa Tanzania na Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Samia Suluhu Hassan amesema ni matamanio yake kuona Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linakuwa la kisasa lenye kuwalea vijana katika uzalendo.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Julai 10,2023 wakati akihutubia wananchi katika kilele cha miaka 60 ya JKT katika uwanja wa Jamhuri Dodoma huku akiongeza kuwa vijana wanaotoka JKT wanapaswa kuwa wazalendo katika nchi yao na hata wanaobaki katika majeshi na vyombo vya ulinzi wawe watu wenye weledi wa kupigiwa mfano.

Aidha amesema kuwa Serikali iko tayari kusimama na JKT na ikibidi kuwadhamini hata katika mikopo ili waweze kuimarisha vikosi vyao kwenye uzalishaji.

“Katika miradi mikubwa mmefanya vizuri sana ikiwemo ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, sisi Serikali tutaendelea kuwaunga mkono na ikibidi mpate mikopo ili kuongeza nguvu ya uzalishaji tuko tayari kuwadhamini,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema vijana wanaopita JKT wanapaswa kubeba dhima ya uzalendo mioyoni mwao siyo katika midomo kwani jeshi linawafanya vijana kuwa wamoja na wenye kuithamini nchi yao katika kuonyesha uzalendo.

Akizungumzia JKT, Rais Samia ametaka waendelee na malengo yao ya kupunguza umasikini na utegemezi kwani ndiyo malengo makuu na kwamba Serikali itaendelea kuongeza nguvu ya kuwa na idadi kubwa ya vijana wanaopitia mafunzo hayo kuliko idadi ya sasa.


Post a Comment

0 Comments