SERIKALI NA WADAU KUWEKEZA KATIKA KILIMO

Na Mwajabu Hoza, Kigoma.

Halmashauri ya wilaya Kigoma na wadau wa kilimo kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Wote Equality Alliance (TAWEA) linalofanya shughuli zake mkoani Kigoma wameweka mikakati itakayochangia utolewaji wa huduma bora katika sekta ya kilimo ili kuongeza  uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa kutatua changamoto zinazowakwamisha wakulima.


Kauli hiyo imetolewa wakati wa kikao cha majadiliano na watoa huduma ngazi ya wilaya kilichokutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo ili kujadili namna ya kutatua changamoto zinazokabili sekta ya kilimo ikiwemo upungufu wa maafisa ugani, upatikanaji wa mbolea za ruzuku na upatikanaji wa mbegu bora ili kutoa wa huduma bora katika sekta ya kilimo.


Festo Mrina ambaye ni mratibu mradi wa ushiriki wa wananchi katika ushirikishwaji, uwajibikaji na uwazi kwenye kuboresha utoaji huduma bora katika sekta ya kilimo amesema shirika la TAWEA linatekeleza mradi huo kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society (FCS) katika kata tano za Matendo, Kidahwe, Simbo, Bitale na Kalinzi kwa Halmashauri ya wilaya ya Kigoma ikiwa ni mwaka wa pili wa utekelezaji wa miradi huo.


Mratibu mradi alieleza kuwa mradi umefanikiwa kujengea uwezo wajumbe 25 wa kamati za Ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii (SAM) toka vijiji vitano lengwa na mradi ambapio wakulima hao wamejengewa uwezo ili kuongeza uwezo wa wananchi kushiriki na kufuatilia utoaji wa huduma bora  katika sekta ya kilimo kwa vijiji vitano vya Matendo, Kidahwe , Simbo, Bitale na Mlangala vilivyopo halmashauri ya wilaya ya Kigoma.


Aidha mratibu mradi, amesema ili kuboresha shughuli za kilimo inatakiwa wakulima waweze kupata mbolea za ruzuku katika maeneo yao ya vijijini kabla ya msimu wa kilimo kuanza, kupata mbegu bora zitakazowezesha ongezeko la uzalishaji wa mazao, sambamba na kuongeza maafisa ugani katika halmashauri ya wilaya ya Kigoma.

 

“ Halmashauri ya wilaya ya Kigoma ina maafisa ugani 16 ambao  wanatakiwa kutoa huduma za ugani kwa  wakulima katika vijiji 46 kuwapatia elimu bora ya kilimo , matumizi ya mbolea lakini pia kutoa ushauri kwa wakulima umuhimu wa skimu na uboreshaji wa miundombinu” alisema.


Afisa kilimo wilaya ya Kigoma Shida Selemani amesema serikali inaendelea kuboresha sekta ya kilimo kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kisekta ikiwemo Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo awamu ya II (ASDP II), kuboresha huduma za ugani, Ruzuku ya pembejeo za Kilimo, hamasa ya vikundi vya kilimo pamoja na kuboresha AMCOS.


Amesema katika wilaya ya Kigoma pia mikakati mingine ambayo inaendelea kutekelezwa ni pamoja na kuhakikisha skimu zilizopo zinaendelea kuboreshwa ikiwemo pia skimu ya  Mkuti pamoja na kufufua skimu mpya ambazo zitasaidia kuwepo kwa kilimo endelevu pamoja na serikali kuendelea kuboresha upatikanaji wa mbolea kulingana na hali ya uchumi kwa wakulima.


 “Bado tuna mabonde ambayo yanahitajika kuendelea kuboreshwa na kwa wilaya ya Kigoma tuna skim ambazo bado zinatumika kienyeji hazina maboresho na hilo linatokana na  changamoto ya ufinyu wa bajeti ili kuweza kuongeza skimu nyingine na kwa sasa ipo skimu moja ya Mkuti ambayo hata yenyewe bado miundombinu yake haijakamilika” alisema Shida.


Jeremia Nicholaus ni mkulima kutoka kijiji cha Kidahwe amesema licha ya jitihada za serikali kuweka mikakati ya uboreshaji wa kilimo bado wakulima wengi hawana uelewa wa kutosha wa matumizi bora ya pembejeo na matumizi ya mbolea na hivyo kuchangia wakulima kulima kilimo kisicho na tija katika uzalishaji wake ambapo ameiomba serikali kuongeza jitihada ya elimu kwa wakulima ili kutatua changamoto hizo.


Aidha,  ameiomba  serikali katika msimu wa kilimo  2023/24 kuhakikisha inasogeza huduma ya mbolea karibu na wananchi ili kuondoa changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata mbolea bila mafanikio na kumwongezea mkulima gharama za uzalishaji.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Mlangala, Ahmadi Buteme amesema shirika la TAWEA limekuwa msaada katika maeneo yao kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kutambua wajibu wao katika ushiriki wa mipango ya kilimo bora pamoja na wananchi kutambua umuhimu wa kuhudhuria mikutano ya kijiji ili kuibua changamoto ambazo serikali inaweza kuzifanyia kazi.


Sanjari na hilo ameiomba serikali kuendelea kutoa ajira kwa Maafisa ugani ambapo katika kata ya Kalinzi yenye vijiji vitano  wana afisa ugani mmoja ambaye anahudumia vijiji zaidi ya vitano na mahitaji ya wananchi ni makubwa  ukilinganisha na idadi ya wataalamu hao.

Post a Comment

0 Comments