ULAJI USIOZINGATIA MAKUNDI MAALUMU YA VYAKULA CHANZO CHA UTAPIAMLO KIGOMA

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Ulaji usiozingatia makundi Maalum ya vyakula yenye virutubisho muhimu kwa Afya, umetajwa kuchangia kuendelea kuwepo kwa hali ya utapiamlo, uzito pungufu, ukondefu na udumavu kwa watoto mkoani Kigoma.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Mhe. Albert Msovela wakati akizungumza kwenye Kikao Jumuishi cha Lishe Ngazi ya Mkoa kilichofanyika katika Ukumbi wa  Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma Leo Julai 10, 2023.

Amesema Mkoa unazalisha vyakula lishe vya kutosha lakini bado kumekuwepo na changamoto ya utapiamlo mkali pamoja na udumavu unaoathiri watoto kutokana na Jamii kushindwa kuzingatia kanuni na taratibu za kupata mlo kamili.

‘’Nitoe wito kwa wataalam wa Afya, ongezeni nguvu katika kutoa Elimu ya Lishe kupitia majukwaa mbalimbali ili wananchi waweze kutambua umuhimu wa kula mlo kamili wao wenyewe pamoja na kulisha watoto wao kwa lengo la kukabiliana na kupunguza changamoto ya utapiamlo na udumavu mkoani hapa’’ amesisitiza Msovela. 

Pia Msovela ameuelekeza Uongozi wa Idara ya Elimu kuhakikisha utaratibu wa wanafunzi kupata chakula shuleni unatekelezwa kwa Asilimia mia moja pamoja na kufuatilia ili kufahamu hali ya ubora wa chakula kinacholiwa na wanafunzi katika Shule za Sekondari za Bweni zilizopo mkoani hapa.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Leba amesema Idara ya Afya kupitia wataalam wa Lishe wameendelea kutoa Elimu ya utambuzi, uandaaji, utunzaji na ulaji wa makundi mbalimbali ya vyakula ili kudumisha utamaduni wa kula mlo kamili.

Amesema iwapo walaji watatambua na kuzingatia umuhimu wa kula vyakula kwa kuzingatia makundi mbalimbali yenye virutubisho Muhimu, wataachana na tabia ya kula vyakula kutokana sababu ya urahisi au wingi katika upatikanaji bali watazingatia mahitaji muhimu ya kiafya mwilini. 

Akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Afua za Lishe, Afisa Lishe Mkoa James Ngalaba amesema hali ya udumavu kimkoa kwa Mwaka 2022 ilikuwa ni watoto 119,864 sawa na asilimia 27.1, udumavu uliokithiri watoto 38,480 sawa na Asilimia 8.7, uzito pungufu 53,961 sawa na Asilimia 12.2, pamoja na ukondefu ikiwa ni watoto 11,057.6 sawa na Asilimia 2.5.

Post a Comment

0 Comments