WAZIRI UMMY AAGIZA HUDUMA ZA NICU ZIWEPO KWENYE HOSPITALI ZOTE ZA HALMASHAURI


Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
Waziri wa Afya Mhe. @ummymwalimu amezitaka Hospitali zote za Halmashauri nchini kuwepo na huduma za uangalizi Maalum kwa Watoto Wachanga (NICU).

Waziri Ummy ametoa agizo hilo Julai 13, 2023 alipokuwa anaongea na timu ya usimamizi wa Afya ya Mkoa, Wataalam wa Afya ngazi ya Jamii pamoja na Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga.

“Katika Mkoa huu wa Shinyanga kuna Hospitali za Halmashauri Sita na Vituo vya Afya vya Serikali 22, haiwezekani kuwepo na huduma za uangalizi maalum kwa watoto wachanga kwenye Halmashauri Mbili tu, Hapana hili mkalifanyie maboresho haraka”. Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amenunua vifaa vya Bil. 6.3 kwa ajili ya huduma za uangalizi maalum kwa watoto wachanga (NICU) katika Mkoa wa Shinyanga. 

“Sasa ni jukumu letu kuimarisha huduma za watoto wachanga ili mama mjamzito akienda kujifungua basi inapendeza sana atoke na mtoto wake”.

Waziri Ummy ameongeza kusema kuwa, hata mtoto akizaliwa na gram 500 anapaswa kuishi.

 “Jana nilikua Maswa, Simiyu kuna mtoto alizaliwa na gram 600 hadi ndani ya siku 10 ana kilo 1 na gram 200, kwakweli tusikubali kupoteza watoto kizembe”. Amesema Waziri Ummy.

Post a Comment

0 Comments