JAMII YASHAURIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUONGEZA UZALISHAJI

Na Mwandishi Wetu, Tabora
Jamii imeshauriwa kutumia mbinu na maarifa mapya pamoja na kujiimarisha katika matumizi ya Teknolojia ili kuongeza Tija  katika uzalishaji mali na kujiletea Maendeleo. 

Wito huo umetolewa Leo Agosti 8, 2023  na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipozungumza kwenye kilele cha Maonesho Sikukuu ya wakulima Nane nane Kanda ya Magharibi, yaliyofanyika mkoani Tabora. 

Amesema jamii inapaswa kutumia zana za kisasa kuemdesha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo matumizi ya Mashine pamoja na kujiimarishia maarifa ya kiutendaji, hali itakayosababisha ongezeko katika kiwango cha uzalishaji pamoja na kupandisha Thamani ya bidhaa zitakazozalishwa. 

Ameeleza kuwa  Serikali ya Awamu ya Sita  imedhamiria kukuza Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kuanzisha majukwaa ya uwekezaji, kuongeza Bajeti za Wizara hizo pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati kwenye nyanja za kiuchumi kwa lengo la kuzidi kuifungua Kanda ya Magharibi. 

"Nimefurahishwa na uwepo wa ongezeko la idadi ya vikundi  vinavyojihusisha na uboreshaji wa Mnyororo wa Thamani kwa mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, hivyo msisite kutumia fursa ya uwepo wa Masoko ya ndani na nje  ya nchi kujinufaisha na kujiimarisha kiuchumi" amesisitiza Andengenye. 

Aidha kiongozi huyo ametoa Rai kwa wakulima kuepuka hasara kwa kuendelea kuviamini na kuvitumia vyama vya Ushirika(AMCOS) kuuza mazao kwa bei zenye tija ili kufikia malengo ya kimaendeleo waliyojiwekea. 

Kadhalika Andengenye amezipongeza Taasisi pamoja na watu binafsi waliojitokeza kushiriki katika maonesho hayo na kuwahimiza wadau hao kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi ili kukuza Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ndani na nje ya mikoa ya Tabora na Kigoma. 

Kilele cha Maadhimisho hayo kimefanyika katika viwanja vya Ipuli Manispaa ya Tabora mkoani humo na kuhudhuriwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Peter Serukamba, Mwenyekiti wa CCM (M) Tabora, Makatibu Tawala (M)Tabora na Kigoma, wakuu wa wilaya, wenyeviti na wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya Tabora na Kigoma, wawakilishi wa Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, watendaji wa Halmashauri za wilaya na Ofisi za wakuu wa mikoa Kigoma na Tabora

Post a Comment

0 Comments