KIONGOZI WA MBIOZA MWENGE AHIMIZA UTUNZAJI WA MAZINGIRA BUHIGWE

Na Editha Karlo,Buhigwe
KIONGOZI  wa mbio za mwenge uhuru kitaifa Abdallah Shaibu Kaim amewataka wananchi wa Wilaya ya Buhigwe kutunza mazingira kwa kupanda miti mbalimbali ili kuhifadhi na kutunza uoto ya asili.

Kiongozi huyo ameyasema  hayo wakati mwenge wa uhuru 2023 ulipofika eneo la Ruheta kwenye mradi wa kupanda miti zaidi ya elfu mbili ikiwa ni mradi wa tisa kati ya miradi kumi iliyotembelewa na mwenge katika Wilaya hiyo.

Amesema utunzaji wa mazingira ni kitu muhimu katika nchi kwani mazingira yanachangia kuleta maendeleo ya nchi pamoja na kutunza uoto
wa asili.

“Niendelee kuwasisitiza wananchi kuendelea kupanda miti katika vyanzo vya maji kwa wingi ili kuondoa tatizo la ukosefu wa maji safi na salama kwenye maeneo yenu”amesema kaim

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Maico Ngayalina amewahakikishia wakimbiza mwenge kuwa wataendelea kutunza vyanzo vya maji kwa kuhamasisha wananchi kupanda miti ili kuvitunza vyanzo hivyo.

Awali akisoma taarifa ya miradi wakati wa kupokea mwenge wa uhuru uliokuwa ukitokea katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mji katika kijiji cha Kasumo Mkuu wa Wilaya Buhigwe Kanali Maico Ngayalina amesema mwenge wa uhuru 2023 utakimbizwa kwa takribani kilomita 105 katika miradi 10 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.721.

Amesema katika miradi hiyi miwili itafunguliwa, minne itazinduliwa, mitatu itawekewa jiwe na mawe ya msingi, huku mingine miwili ikitembelewa na kukaguliwa.

Mkuu wa Wilaya aliitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa barabara ya Lami yenye urefu wa kilomita 1.874, Majengo mawili ya madarasa katika shule ya msingi Kibuye, Klabu ya wapinga rushwa shule ya msingi Mnyegela, ukaguzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe.

Miradi mingine ni pamoja na upandaji wa miti zaidi ya elfu mbili, usafi katika soko la Muyama, uzinduzi wa klabu ya wapinga rushwa shule ya msingi Kibuye, kukabidhi pikipiki kwa kikundi cha vijana na mradi wa kitalu cha utunzaji miche ya miti.

Post a Comment

0 Comments