KIWANGO CHA UDUMAVU CHAPUNGUA MKOANI KIGOMA

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkoa wa Kigoma umefanikiwa kupunguza Kiwango cha Udumavu na Utapiamlo mkali kutoka Asilimia 47 hadi kufikia 27 katika kipindi cha kuanzia  Mwaka 2020 hadi 2023. 

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipozungumza kwenye Kikao cha Tathimini ya Lishe Mkoa, na kusisitiza kuwa mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na Jamii kujengewa uelewa kuhusu umuhimu wa kuzingatia kanuni za Afya ikiwemo kula makundi mbalimbali ya vyakula.

Amesema kuendelea kupungua kwa changamoto hiyo kutafanikisha makuzi bora ya watoto pamoja na kujenga jamii yenye ustawi  mzuri kiafya  itakayoimarisha uchumi wa mkoa wa Kigoma. 

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Albert Msovela amewaelekeza Maafisa Lishe katika Halmashauri zote za Mkoa kufuatilia ubora wa chumvi inayouzwa kwenye masoko mkoani hapa. 

"Wataalam wa Lishe Fuatilieni katika Masoko ili muweze kubaini iwapo chumvi  inayouzwa ina madini joto, hii itasaidia kuimarisha usalama wa Afya za walaji" amesema Msovela.

Kikao hicho kimehudhuriwa na  wakuu wa Wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga wakuu na Maafisa lishe wilaya pamoja na Wataalam kutoka Sekretariet ya Mkoa wa Kigoma.

Post a Comment

0 Comments