MKUU WA MKOA WA KIGOMA AWASISITIZA VIONGOZI WA DINI KUENDELEA KUHUBIRI AMANI

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amekutana na viongozi wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste (CPCT)Mkoa wa Kigoma na kuwasisitiza kuendelea kuhubiri Amani na Upendo kwa lengo la kudumisha mshikamano na kuchochea Maendeleo ya Mkoa. 

Kupitia kikao hicho, Andengenye ameitaka jamii kuachana na imani za kishirikina hali inayosababisha uwepo wa matukio ya upigaji wa Ramli chonganishi (Lambalamba) na kusababisha uvunjifu wa Amani na utulivu katika baadhi ya maeneo mkoani hapa.

Aidha Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi kutoa Taarifa mapema wanapobaini uwepo wa viashiria vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao ili Serikali iweze kuchukua hatua dhidi ya wahusika  kwa lengo la kudumisha ufuasi wa Sheria.

Nao viongozi hao wamemshukuru Andengenye kwa ushirikiano mzuri  anaoendelea kuwapa, jambo linalotoa fursa kwao kuiunganisha Serikali na waumini wa madhehebu wanayoyaongoza mkoani  hapa.

"Ushirikiano unaotupa umetufanya tuwe huru kujadili kwa pamoja masuala mbalimbali yanayowagusa waumini wetu  kama sehemu ya jamii, pamoja na kufikia tatuzi za baadhi ya changamoto zinazotukabili katika maeneo tunayoyaongoza" wamesisitiza viongozi hao wa kidini.

Post a Comment

0 Comments