USHIRIKI WA MASHUJAA FC LIGI KUU TANZANIA KUONGEZA CHACHU YA MAENDELEO KIGOMA

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema ushiriki wa Timu ya Mashujaa FC katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara utaongeza chachu ya Maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Kigoma. 

Andengenye ametoa kauli hiyo alipotembelea na kukagua Maendeleo ya Ukarabati wa Uwanja wa CCM Lake Tanganyika Stadium utakaotumiwa na Timu ya Mashujaa kwa ajili ya michezo ya nyumbani katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara Msimu wa 2023/2024. 

Ameeleza kuwa, kutokana na ushiriki wa timu hiyo, Mkoa utapokea wageni kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kushuhudia michezo ya ligi kuu ambapo kuanzia wafanyabiashara wakubwa  hadi wajasiriamali wadogo watapata fursa ya kunufaika kiuchumi kutokana na kuwahudumia wageni hao. 

"Pamoja na kupata burudani, michezo inatoa fursa  mbalimbali za kujiimarisha kiuchumi kupitia biashara, nitoe wito kwa wafanyabiashara na wakazi kwa ujumla tuchangamkie fursa za kiuchumi zitakazojitokeza ambazo zitatokana na wageni watakaokuja kwa ajili ya kushuhudia michezo mbalimbali ya ligi kuu" amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa. 

Upande wake Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa  Kigoma, Mha. Francisco Magoti amesema ukarabati huo unahusu maeneo ya majukwaa, vyumba vya kubadilishia nguo kwa wachezaji, ukumbi wa mikutano, vyoo pamoja na eneo la kuchezea mpira. 

" Mafundi wapo kazini na tutahakikisha  maboresho muhimu yanakamilika kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi kuu Tanzania Bara ili kuruhusu michezo ifanyike kama ilivyopangwa huku uwanja ukiwa katika ubora unaotakiwa" amefafanua Magoti. 

Upande wake Afisa Vijana Mkoa wa Kigoma,  Edward Manase amesema  wameridhishwa na maendeleo ya kazi mbalimbali zinazofanyika za marekebisho ya uwanja huo  huku akiwahimiza watendaji  kutanguliza uzalendo na kuzingatia ubora.

Post a Comment

0 Comments