VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUKEMEA UNYANYASAJI WA KIJINSIA

Na Glory Enock, Kigoma
Viongozi wa dini katika Halmashauri ya Wilaya Kigoma wametakiwa kuendelea kutumia nafasi zao kuhimiza jamii kuachana na vitendo vya ukatili ambavyo vimeendelea kushamili kwenye jamii hasa kwa wanawake na watoto.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa ustawi wa jamii Halmashauri ya Wilaya Kigoma Bw. George Sauli, wakati wa Mdahalo uliowakutanisha ofisi ya ustawi wa jamii na viongozi wa dini na wananchi wa Kata ya Kagongo, ambapo amesema ukatili umeendelea kufanyika kutokana na jamii kutokuwa na hofu ya Mungu na hivyo viongozi wa dini ni wajibu wao kuelimisha waumini wao ili kuachana na unyanyasaji huo.

Amesema ni wakati sasa kila mtu kutoa taarifa na kuwa mlinzi kwa watoto ambao wameonekana kuwa wahanga wa vitendo vya  ukatili kila kukicha.

"Watoto wanabakwa na wanaofanya ubakaji huo ni ndugu, jamaa, na marafiki wa karibu, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunawalinda na kuwasaidia kwa kutoa ushirikiano pale tunapohitajika kutoa taarifa za vitendo hivyo’.

Baadhi ya viongozi wa Dini kutoka Kata ya Kagongo Hamashauri ya Wilaya Kigoma wamesema kuwa wataendelea kuwakumbusha wazazi na walezi kutambua wajibu wao katika kuwahudumia watoto na familia zao kwa ujumla kwani kushindwa kuhudumia familia ni miongoni mwa sababu za vitendo vya ukatili kuendelea kuwepo.

Aidha wamesema ukosefu wa hofu ya Mungu ndio chanzo kikubwa zaidi kwa jamii kushindwa kuogopa na kufanya ukatilii ambao umeendelea kuwa na madhara makubwa kwa wahanga ambao ni watoto na wanawake.

Kwa upande wao wazazi na walezi waliojitokeza kwenye mdahalo huo wamesema migogoro kwa wanandoa imechangia kwa kiasi kikubwa watoto kufanyiwa ukatili kwani mama na baba wanapogombana watoto wanabaki bila uangalizi na hivyo kujikuta katika mazingira ambayo si rafiki.

Naye Afisa maendeleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Minza Edward amesema mifumo dume imeendelea kuathiri familia nyingi kwani husababisha wanawake kubaki kulea familia huku wanaume wao wakiwa hawajali wajibu wao katika familia pamoja na ukosefu wa maadili.

Mafunzo hayo yana lenga kuikumbusha jamii kuendelea kupiga vita ukatili kwenye jamii na yameendeshwa kwa kushirikiana na shirika la watoto duniani UNICEF yakiwakutanisha viongozi wa dini kuwakumbusha wajibu wao kwa jamii ili iweze kubadilika na kuachana na vitendo vya unyanyasaji.

Post a Comment

0 Comments