WAHANDISI KIGOMA WAHIMIZWA KUSIMAMIA MIRADI

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2023 Abdallah Kaim amewaelekeza Wahandisi katika Halmashauri za Mkoa wa Kigoma kuweka utaratibu  endelevu wa kufuatilia na kukagua miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao. 

Kaim ametoa maelekezo hayo mara baada ya kukagua Mradi wa ujenzi wa madarasa manne katika Shule ya Sekondari Buha iliyopo wilayani Buhigwe na kusisitiza kuwa dosari ndogondogo zilizobainika katika miradi iliyotembelewa zimetokana na wahandisi kutokufuatilia kwa ukaribu zoezi la ujenzi wa baadhi ya miradi ya maendeleo katika maeneo yao ya kiutendaji. 

‘’Hatutegemei kuona dosari ndogondogo zikiendelea kuonekana mara baada ya miradi kukamilika, hii ni ishara kuwa kuna baadhi ya wahandisi  hawatekelezi ipasavyo zoezi la kukagua hatua mbalimbali za utekelezaji wa baadhi ya miradi’’ Amesema Kaim.

Mwenge wa Uhuru wilayani Buhigwe umetembelea mradi wa Hifadhi ya Mazingira katika Shule ya Msingi Kahimba, kuweka Jiwe la Msingi Zahanati ya kijiji Kasumo, Nyumba ya Makazi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe pamoja na  Barabara ya Lami Buhigwe mjini. 

Kadhalika Mwenge huo umezindua madarasa manne katika Shule ya Sekondari Buha, mradi wa pikipiki za kusafirisha abiria Kijiji cha Kasumo, ujenzi wa Tanki la Maji kijiji cha Songambele pamoja na kushiriki zoezi la kupanda miti katika kijiji cha Ruheka. 

Miradi yote ikiwa na Thamani ya Shilingi Bil. 3.6 imepokelewa na Mwenge huo wa Uhuru.

Post a Comment

0 Comments