WANANCHI WAIOMBA MAHAKAMA KUZUIA UFANYWAJI WA TAMTHIMINI ILI KUWAONDOA KATIKA MAENEO YAO








Na Emmanuel Matinde, Kigoma

Mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa kijiji cha Kalilani wilayani Uvinza mkoani Kigoma na serikali uliodumu kwa zaidi ya miaka 30 umechukua sura mpya baada ya wananchi hao kuwasilisha mahakama kuu kanda ya Kigoma maombi madogo wakiiomba mahakama hiyo iweke zuio kuwazuia bodi ya wadhamini wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya tathimini ikiwa ni hatua ya mwanzo ya kutaka kuwaondoa katika maeneo yao.

Kumekuwepo na ugomvi wa muda mrefu wa kubishania mipaka baina ya TANAPA kwa upande mmoja na wananchi wa kijiji cha Kalilani kwa upande mwingine, TANAPA wakisema wananchi kijiji cha Kalilani hasa vitongoji viwili vya Mahasa na Kabukuyungu wanaishi ndani ya hifadhi ya Milima ya Mahale wakati wananchi wao wanaona wako nje ya hifadhi.

Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale ilianzishwa mwaka 1985 kupitia tangazo la serikali namba 262 ambalo liliainisha mipaka ambapo wananchi wanasema kwa mujibu wa mipaka hiyo wao wako nje ya hifadhi huku TANAPA kwa upande mwingine wanasema wananchi hao wako ndani ya hifadhi.

Kutokana na sintofahamu hiyo wakati serikali ikiwa imeanza kufanya tathimini ya maeneo hayo ili kuwaondoa wananchi Winfrida Batholomeo na wenzake 91 wakisimamiwa na Wakili Gastoni Garubindi, wamepeleka maombi madogo ya kuomba serikali pamoja na TANAPA wasitishe kufanya zoezi lao la kufanya tathimini wakati wakisubiri kupeleka shauri la msingi mahakamani ambalo litaamua mipaka halisi ya hifadhi ni ipi ili wananchi kama wako nje ya hifadhi waendelee na shughuli zao au kama wako ndani ya hifadhi basi utaratibu mwingine wa kuwaondoa uweze kuendelea.

Maombi hayo yamepelekwa mahakamani hapo chini ya kifu cha pili kifungu kidogo cha tatu cha sheria inayoitwa Judicature And Application of Laws Act kwa kifupi (JALA), iliyorithiwa kutoka Uingereza ambayo inatumiwa pia na nchi za Jumuiya Madola zilizokuwa chini ya koloni la Mwingereza.

Mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Jaji Lameck Mlacha, anayesikiliza shauri hilo namba 37 la mwaka 2023 waleta maombi wameiomba mahakama hiyo kuona umuhimu wa kutoa amri ya zuio hilo ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kuwapata wananchi hao kutokana na kuwaondoa katika maeneo hayo wakati shauri lao la msingi likiwa bado kusikilizwa.

Aidha Wakili wa upande wa waleta maombi Gastoni Garubindi, ameieleza mahakama kuwa kwa mujibu wa nyaraka zilizopo kijiji cha Kalilani kilisajiliwa kama kijiji mwaka 1995 kwa sheria ya serikali za mitaa.  

Kwa upande wa Jamhuri inayowakilishwa na mawakili wawili katika shauri hilo, Anord Simeon na Nickson Tengesi na mawakili wawili upande wa TANAPA Benard Mganda na Celestine Mgai imesisitiza kuwa wananchi hao wako ndani ya hifadhi hivyo kuiomba mahakama isitoe zuio lolote kwa kile walichodai kuwa mipango yao itachelewa.

Baada ya majumuisho ya hoja za pande zote mbili mahakama ilisema itatoa uamuzi huo mdogo mnamo Agosti 15 mwaka huu saa tano kamili asubuhi.

Awali zaidi ya wananchi mia moja wakiwemo wanawake kumi wenye watoto wachanga 12 na wajawazito wanne, walisafiri kwa boti usiku na mchana kwa zaidi ya saa kumi na tano kutoka kijiji cha Kalilani mpaka mjini Kigoma kuwasilisha maombi yao mahakamani hapo kufuatia wito wa mahakama iliyotaka kujiridhisha juu ya uwepo wa malalamiko hayo ili kuepuka changamoto ya watu kudandia mashauri yasiyowahusu

Kikao cha shauri hilo kinatajwa kuwa miongoni mwa vikao vilivyoweka rekodi ya kuhudhuriwa na idadi kubwa ya watu kwa wakati mmoja tangu kuanzishwa kwa shughuli za mahakama kuu kanda ya Kigoma.


Post a Comment

0 Comments