BODI YA NYAMA NCHINI YAZIFUNGIA KWA MUDA BUCHA NA MAENEO 26 YA KUUZA NYAMA YA NGURUWE

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Bodi ya nyama nchini imezifungia kwa muda bucha na maeneo 26 ya kuuza nyama ya nguruwe katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kutokana na wauzaji kutozingatia taratibu za uuzaji wa nyama hiyo hali inayohatarisha afya za walaji.

Afisa Mfawidhi Bodi ya Nyama Tanzania Kanda ya Magharibi Be. Joseph Kulwa amesema pamoja na ukaguzi huo wanawarasimisha wafanyabiashara wa nyama ya nguruwe ili wafanye biashara hiyo kwa kuzingatia sheria ikiwa ni pamoja na kuwa na sare maalum, kupimwa afya, kuwa na leseni, kuwa na mazingira safi na kabati la kutunzia nyama.

Amesema uuzaji wa Nyama unapashwa kuzingatia sheria hivyo wote waliofungiwa wanatakiwa kurekebisha kasoro zote ili waweze kufunguliwa tena na kuendelea na shughuli zao.

Aidha Bw.Kulwa amewataka wananchi kutokubali kula Nyama katika mazingira ya uchafu na kutoa taarifa za wafanyabiashara wanaouza bila kuzingatia USAFI na taratibu zinazotakiwa.
 
Kwa upande wao wadau wa biashara hiyo wameitaka serikali kuwa na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha mlaji anapata huduma bora huku waliofungiwa wakiahidi kukamilisha taratibu zinazotakiwa na serikali ili waendelee kuuza nyama hiyo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa machinjio ya Nguruwe Nyansha wilayani Kasulu Bondo Kahambi ameitaka bodi ya Nyama kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wafanyabiashara ili kuepesha madhara yanayoweza kutokea.

Amesema kwa sasa machinjio hiyo inachinja Kati ya Nguruwe 15 na 20 kwa siku.

Post a Comment

0 Comments