IWAPO RAIS SAMIA ANASIKILIZA KERO ZA WANANCHI, NINYI NI AKINA NANI - MAJALIWA


Na Mwandishi Wetu, Kigoma

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kama Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya ziara na kusilikiliza kero za wananchi, haoni ni kwa nini watumishi wengine wa umma wanashindwa kufanya hivyo.

 

“Iwapo Mkuu wa nchi, Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anaenda kote nchini na kusikiliza wananchi, je ninyi ni akina nani? Nilishasema mtenge siku tatu katika wiki mwende vijijini na kuwasikiliza wananchi,” alisema.

 

Ameyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Septemba 21, 2023) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na mamia ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nguruka, wilayani humo.

 

“Mheshimiwa DC simamia watu wako waende vijijini. Nilishasema hata kama magari ni machache, pangeni ratiba, mbebane na mwende kuwasikiliza wananchi. Gari litawapeleka na kuwaacha kwenye vijiji husika na wakati linarudi litawapitia wote. Nenda mkawasikilize wananchi, nenda mkawatumikie wananchi,” alisisitiza.


Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa sh. milioni 500 za kujenga kituo kipya cha afya katika tarafa ya Nguruka, wilayani Uvinza mkoani Kigoma.

Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na mamia ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nguruka.

Waziri Mkuu amesema uamuzi huo unatokana na ombi la Mbunge wa Kigoma Kusini, Nashon Bindyaguze ambaye amekuwa akilalamikia udogo wa kituo kilichopo ikilinganishwa na idadi ya wakazi wa kata nne zilizopo.

"Mbunge wenu amekuwa akilalamikia udogo wa kituo cha afya kilichopo kwamba kinahudumia watu wengi kuliko uwezo wake. Nimeenda kukikagua, baadhi ya majengo yamechakaa, nimeelezwa zamani ilikuwa ni zahanati."

Post a Comment

0 Comments