MATOKEO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI 2022 YATUMIKE KUTEKELEZA MIPANGO YA MAENDELEO: RAIS UTPC

Na Editha Karlo, Kigoma
MATOKEO ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yametakiwa kwenda kuisaidia jamii kujiletea maendeleo kwa kupanga mipango yao kutokana na takwimu sahihi zinazopaswa kufikishwa na wanahabari weledi katika masuala ya takwimu.

Rais wa umoja wa klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Deogratius Nsokolo ametoa wito huo wakati wa mafunzo ya siku mbili ya wanahabari na kuongeza kuwa endapo wanahabari wataelewa na kwenda kutumia takwimu hizo katika kazi zao itasaidia jamii kufahamu changamoto zao na namna ya kukabiliana nazo.

Nsokolo amesema kuwa matumizi ya matokeo ya sensa yatasaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa kuanzia ngazi ya Taifa hadi chini.

“Niipongeze ofisi ya Takwimu kwa kufanya ushirikishwaji kwa makundi yote  katika sensa ya mwaka 2022, hata mimi nilikuwa mjumbe wa kamati ya sensa ya Mkoa”amesema Nsokolo

Kwa upande wake Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi 2022 Tanzania Bara Anne Makinda ambaye ni Spika mstaafu wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema wataendelea kutoa elimu katika makundi mbalimbali mpaka vijijini ili wananchi nao waweze kupanga na kutekeleza mambo yao.

Amesema wanahabari wanaweza kuisaidia vizuri jamii kujua ni kwa namna gani waweze kufuatilia mahitaji muhimu yanayopaswa kupelekwa kwao kutokana na takwimu kuonesha changamoto zote kila eneo nchini.

“Nyie ni kundi muhimu sana kupitia kalamu zenu mnaweza kuhamasisha jamii kutumia matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ili waweze kupanga na kutekeleza majukumu yao vizuri” amesema Makinda.

Naye  Mtaalamu wa habari na mawasiliano toka ofisi ya Taifa ya Takwimu Said Ameir amesema mafunzo hayo kwa wanahabari yanapaswa kwenda kusaidia jamii kutekeleza shughuli za maendeleo kwa ushahidi wa kitakwimu.

Amesema matokeo ya sensa ya mwaka 2022 yatasaidia kuongeza maamuzi yenye ushahidi wa kitakwimu katika ngazi zote za utawala.

Nao baadhi ya wanahabari kutoka mikoa ya Kigoma wameahidi kwenda kufanyakazi zao kwa weledi mkubwa kwa kutumia takwimu ambazo zitawapa mwanga wananchi kutambua hali ya maendeleo katika maeneo yao.

“Mafunzo haya ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yamekuwa mazuri wawezeshaji wetu wametupitisha vizuri na sisi tutayafanyia kazi” walisema.

Mafunzo hayo yanetolewa kwa waandishi wa habari zaidi ya 70 wa mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi yaliyoandaliwa na ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Ikumbukwe kuwa Sensa ya kwanza ya watu na makazi ilifanyika mwaka 1967 miaka 6 baada ya uhuru na mpaka sasa zimefanyika sensa 6 ikiwa ya mwisho imefanyika mwaka jana 2022.

Post a Comment

0 Comments