WANANCHI WAOMBA KUSOGEZEWA HUDUMA KARIBU NA MAKAZI YAO





Na Mwajabu Hoza , Kigoma

WANANCHI wa eneo la Kigamboni mtaa wa Butunga kata ya Kibirizi Manispaa ya Kigoma ujiji wameiomba serikali iweze kuwapatia kibali cha kutekeleza ujenzi wa shule ya msingi katika eneo lao ili kuwanusuru watoto wao na ajali zinazoweza kutokea wakati wakienda shule eneo ambalo ni mbali na makazi yao.

 

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara wananchi hao wamemuomba mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli  kufika eneo hilo ili waweze kufikisha changamoto zao zinazo wakabili ikiwemo ukosefu wa shule, huduma za afya, miundombinu ya barabara pamoja na soko.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Butunga Hamisi Yasini anaeleza kero ya ukosefu wa shule ya msingi eneo la Kigamboni kuwa inaathiri watoto wa eneo hilo kutokana na umbali wanaotembea kufuata shule wanalazimika kuvuka barabara na hivyo wazazi kuhofia usalama wa watoto wao.

 

“ Shule zipo mbali na maeneo wanayoishi wananchi na mwezi wa nane mtoto mmoja alipoteza maisha wakati akivuka kuelekea shule hivyo uwepo wa shule katika eneo lao ni muhimu sana kwetu” amesema Yasini.

 

Telesia Revocatus anaeleza kuwa hayo ni makazi mapya bado hayajafikiwa na huduma zote muhimu ambazo ni hitaji kubwa kwa wananchi wanaoishi katika eneo hilo la kigamboni hivyo wanaiomba serikali iweze kuwasaidia kupata huduma za afya, soko, shule na miundombinu ya barabara.


Baada ya maombi hayo ya wananchi, Mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli imemlazimu kufika eneo ambalo wananchi wamelitenga kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi ambapo mara baada ya kuliona aliwataka wananchi wawe watulivu  kwa kuwa hitaji la shule ni muhimu na yupo tayari kushirikiana na wananchi katika ujenzi huo.

 

“Namuagiza mkuu wa idara ya ardhi aweze kufika katika eneo la ujenzi wa shule na kulipima na kuja kunipa taarifa kama linatosheleza kwa ujenzi wa shule na kama limepungua tuwaombe wenyeji wa karibu na eneo mlilolitenga ili kuzungumza nao na kuongeza eneo hilo ili ujenzi uweze kuanza” amesema

 

Lakini pia mkuu huyo amewataka wenyeviti wa mitaa kuitisha mkutano na kuzungumza na wananchi ambao wapo tayari kutoa maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa soko na Zahanati kwa kufanya nao makubaliano ya kuwalipa kiasi kidogo ili kuwezesha upatikanaji wa huduma hizo muhimu.

 

Asilimia kubwa ya wakazi wanaoishi katika eneo la Kigamboni walihamia makazi hayo mara baada ya kupisha ujenzi wa bandari kavu ya katosho.

Post a Comment

0 Comments