ANDENGENYE AFUNGUA SOKO LA KIMKAKATI MUNANILA BUHIGWE MKOANI KIGOMA






Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye  amefungua soko la kimkakati Munanila, lililopo wilayani Buhigwe Mkoani hapa. 

Ufunguzi wa Soko hilo lililojengwa kwa Thamani ya Shilingi Bil. 2.5 fedha kutoka Serikali Kuu, umefanyika Leo Oktoba 12, 2023 huku ukienda sambamba na ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa iliyolenga kukagua Miradi ya Maendeleo pamoja na kusikiliza kisha kutatua kero za Wananchi. 

Akizungumza na wakazi waliojitokeza kwenye ufunguzi wa soko hilo lililopo mpakani mwa Tanzania na Burundi, Andengenye ametoa wito kwa wanufaika wa mradi huo kuitumia vizuri fursa hiyo kujiimarisha kiuchumi. 

Kiongozi huyo amepokea  changamoto za uendeshaji wa soko hilo na  kuuelekeza uongozi wa soko kuzingatia uwazi na ushirikishwaji ili kuondoa malalamiko yanayojitokeza miongoni mwa wafanyabiashara. 

Pia amewasisitiza wafanyabiashara hao kuendelea kuchangia makusanyo ya Halmashauri kupitia soko hilo ili kuiwezesha serikali kufanya maboresho ikiwemo upanuzi wa miundombinu ya soko na kutoa fursa ya ongezeko la  wafanyabiashara  katika eneo hilo. 

Akiwasilisha Taarifa ya Maendeleo ya ujenzi wa Soko la kimkakati Mnanila, Mkuu wa Sehemu ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji wilaya ya Buhigwe Onesphory John, amesema ujenzi wa soko hilo umelenga kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka nchi hizo mbili ili kuongeza chachu ya ukuaji wa biashara katika eneo hilo. 

Taarifa hiyo imefafanua kuwa jumla ya vibanda 144 vimekamilika na tayari wafanyabiashara mia moja wamekamilisha taratibu za Zabuni za upangishwaji kisha kupatiwa vibanda vya biashara. 

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa ameiasa jamii kujenga utamaduni wa kupima Afya mara kwa mara ili kuepuka usugu wa maradhi na kusababisha baadhi yao kuamini kuwa wanatendewa vitendo vinavyohusiana na imani za  kishirikina . 

"Jengeni tabia ya kupima Afya ili mtambue maradhi yanayowasumbua kwa muda mrefu jambo linalosababisha mjiingize katika imani za kishirikina na kukimbilia ramli chonganishi au kwa kina kamchape, achaneni nao hao watu ni wezi tu" amesisitiza Andengenye.

Kadhalika amewakumbusha wakazi  wilayani humo kuendelea kutunza Mazingira kwa kupanda miti rafiki kwa vyanzo vya maji.

Post a Comment

0 Comments