BOT YAWATAKA WAFANYABISHARA WANAOBADILI FEDHA KUFUATA KANUNI MPYA

Washiriki wa mafunzo ya usalama na fedha yaliyotolewa na BoT kwa lengo la kuwataka wafanyabiashara wengi wa Kigoma kutumia fursa ya kuwekeza katika biashara ya kubadilisha 
fedha za kigeni.

Amri Mbalikali meneja wa kitengo cha uchunguzi cha BoT akitoa ufafanuzi kwa upatikanaji wa leseni za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni 


Na Adela Madyane, Kigoma
Benki kuu ya Tanzania (BoT) imetoa wito kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Kigoma kubadili fedha za kigeni ( Bureaux de Change) kwa kufuata kanuni mpya za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ya mwaka 2023 zilizowekwa katika madaraja matatu na kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali namba 729 la Oktoba 6, 2023.

Wito huo umetolewa na Amri Mbalikali meneja wa kitengo cha uchunguzi cha BoT wakati akitoa elimu kwa Jeshi la polisi, wafanyabiashara na wamiliki wa hoteli mkoani humo na kuwataka kufuata kanuni zinazotolewa na BoT na si kupitia kwa vishoka na njia nyingine zisizo sahihi zinazoleta madhara katika jamii.

"Kanuni zimerahishwa daraja A ni duka linalomilikiwa na wageni au wazawa, mgeni anapaswa kuwa na mtaji wa fedha za Kitanzania bilioni moja na mwenyeji kuwa na milioni 500, daraja B ni kwaajili ya wazawa wa mtaji wa milioni 200 na daraja C ni duka lililoanzishwa na hoteli yenye hadhi ya nyota tatu au zaidi kwa ajili ya kufanya miamala ya papo kwa papo kwa wateja wa hoteli tu ambapo leseni yake itatolewa kwa hoteli" amefafanua hayo Mbalikali.

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma ACP Filemon Makungu, amewaelekeza wafanyabiashara ya kubadilisha fedha kuimarisha ulinzi katika maeneo ya kubadilisha fedha za kigeni kwa kuweka askari wa ulinzi wenye mafunzo kwani biashara ya kubadili pesa inahusisha pesa na si bidhaa hivyo kuwa na ulinzi ni lazima kwaajili ya kukuza uchumi wao na wa nchi kwa ujumla.

Naye Omary Msuya afisa wa BoT kitengo cha usimamizi wa fedha amesema pamoja na mambo mengine mafunzo hayo yametolewa kwa lengo la kuvutia wafanyabiashara wengi zaidi kuomba leseni kwaajili ya kuanzisha maduka ya kubadilisha fedha na wale wanaofanya biashara hiyo kwa kujificha waweze kurasimisha ili kusaidia kuendesha uchumi wa nchi na kwamba watakaoendelea kufanya kwa kificho hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Nae Lois Ntibilaba ambaye ni mmiliki wa hoteli ya Mahale iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji amesema elimu waliyoipata itawawezesha wengi kujiunga na biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kwasababu kiwango cha chini cha milioni 200 wengi wanacho na kuiomba serikali iendelee kutoa elimu kwa watu wengi waelewe na kutumia fursa za kimpaka ili wajiunge kwenye biashara hiyo.

Post a Comment

0 Comments