POSTA KIGOMA KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA






Na Mwajabu Hoza , Kigoma.
SHIRIKA la posta Mkoa wa Kigoma limeeleza kuendelea kuboresha huduma zao kwa njia ya kidigitali ili kwendana na kasi ya teknolojia , kukabiliana na ushindani kutoka katika makampuni mengine pamoja na kukidhi mahitaji ya wateja wanaotumia huduma hizo.

Kauli hiyo imetokewa na Meneja wa Shirika la Posta Mkoa wa Kigoma Paul Mshanga wakati wa kuadhimisha siku ya Posta duniani ambayo huadhimishwa Octoba Tisa ya kila Mwaka.

Amesema Shirika la posta linaendelea kuboresha huduma zake ili kwendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani pamoja na kuingia katika ushindani wa  makampuni na taasisi za usafirishaji kwa kuongeza ufanisi zaidi kwenye huduma za usafirishaji kwa njia ya mtandao.

" Tuna magari ambayo yanasafirisha mizigo mikubwa lakini pia tumeimarisha mifumo yetu  kimtandao tuna huduma ya duka mtandao hii  mwananchi anaweza kuagiza mzigo kupitia online posta mtandao akiwa nyumbani kwake na posta tunamfikishia mpaka nyumbani ama kwenye ofisi za posta zilizo karibu na mteja. "Amesema Mshanga. 

Amesema Shirika halijabaki nyuma katika kuendelea kubuni mbinu mbalimbali za usafirishaji wa mizigo lengo ni kuendelea kuongeza idadi ya wateja ambapo pia ameeleza kuwepo kwa App Posta kiganjani ambayo inataarifa zinazohusu huduma za Posta ambapo wananchi wanaweza itumia kupata huduma. 

Afisa Masoko Mwandamizi Ndagije Chobariko anasema uboreshaji wa huduma za Posta kwa wateja wa ndani na nje ya nchi umeongeza uaminifu kwa kwa wananchi ambapo idadi ya wanaotumia huduma hizo imeongezeka kwa Kasi.

Ndagije anasema uboreshaji huo wa teknolojia kwa njia ya mtandao pia umeongeza kiwango cha mapato ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kwa mwaka 2022 Shirika lilizalisha  kiasi cha shilingi milioni 612 na mwaka 2023 Hadi mwezi Juni  uzalishaji uliongezeka  kwa zaidi ya asilimia 29 ambapo kiasi cha shilingi milioni 937 zilizalishwa na Shirika hilo Mkoani Kigoma.

Amesema Hadi Sasa shirika la Posta limeendelea kutanua huduma zake katika nchi mbalimbali ambapo kwa Sasa mikoa yote inapata huduma ya usafirishaji pamoja na nchi 192.

Baadhi ya wateja wanaotumia huduma za Shirika hilo Isack Basese anasema huduma zinazotolewa zimekuwa zikiwavutia kutumia huduma hizo lakini pia uhakika wa kufikishiwa mizigo kwa wakati na bila kupotea ama kupungua imekuwa sababu ya wao kuendelea kutumia huduma za Shirika hilo.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya Posta mwaka 2023 ni pamoja kwa uaminifu tushirikiane kwa mustakabali salama na mtandao wa maisha yajayo.

Post a Comment

0 Comments