RAS MSOVELA: ACHENI MAJUNGU CHAPENI KAZI



Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Watumishi wa Umma katika Halmashauri ya Mji Kasulu wametakiwa kuacha tabia za kuendekeza majungu na kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kazi ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi  wao na  kutatua changamoto zinazowakabili wananchi  ili  kuwaletea Maendeleo. 

Kauli hiyo Imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Albert Msovela alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, akiwa katika ziara yake ya kikazi iliyolenga  kusikiliza na kutatua kero za watumishi wa Umma katika Halmashauri Nane za Mkoa wa Kigoma. 

Amesema haridhishwi na tabia za baadhi ya watumishi kutumia muda mwingi kwa ajili ya kusengenyana badala ya kutekeleza wajibu wao,  hali inayosababisha wananchi kukosa huduma sahihi na kwa wakati, katika baadhi ya Ofisi za Umma.

"Kama hamna Umoja, Mshikamano, nidhamu na kushindwa kuzingatia mtiririko wa mipango kazi inayowekwa na Serikali msitegemee kupata matokeo chanya" alisema Msovela. 

Aidha, amewataka watendaji hao kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuiwezesha halmashauri kutekeleza mipango ya Maendeleo. 

Pia amewasisitiza wakuu wa Idara na Vitengo kuongeza ushirikishwaji wa wataaalam walio chini yao katika kufanya maamuzi mbalimbali ya kiutendaji. 

Ziara hiyo imewahusisha wakuu wa Sehemu na Vitengo katika Sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma.

Post a Comment

0 Comments