TRENI YAPATA AJALI KIGOMA, MABEHEWA MATATU YAACHA NJIA





Na Mwajabu Hoza, Kigoma

 

GARI moshi (Treni) iliyokuwa ikitokea Kigoma kuelekea  jijini Dar es Salaam imepata ajali mita chache kutokea stesheni ya mkoa wa Kigoma ambapo mabehewa matatu kati ya 14 yaliyokuwa yamebeba abiria  yaliacha njia katika eneo Kibirizi ndani ya Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma.

 

Tukio hilo limetokea majira ya saa tatu asubuhi treni ya abiria iliyokuwa na abiria 512  iliondoka kituo cha stesheni ya Kigoma Mjini na mara baada ya kufika eneo la Kibirizi mabehewa matatu ya nyuma yaliacha njia na kuelekea eneo la aridhi.

 

Evaristi Mshana ni msaidizi wa stesheni master shirika la reli Kigoma anasema  treni hiyo ilikuwa ikielekea Dar es Salaam ambapo baada ya dakika tano  alipata taarifa ya mabehewa matatu kuhama njia katika eneo la Kibirizi ambapo ni kilomita chache kutokea stesheni.

 

“ Kati ya mabehewa matatu yaliyohama njia moja tu ndio lilikuwa na abiria mabehewa mawili yalikuwa yanatarajia kuchukuwa abiria kituo cha stesheni ya Tabora hivyo tulifanya jitihada ya kuwahamisha  abiria na taratibu za safari ziliandelea ilipofisa majira ya saa nne asubuhi” amesema

 

Mshana amesema katika tukio hilo hakuna abiria aliyepata madhara yoyote wala mali zao ambapo taratibu za kufanya uchunguzi zinaendelea ili kujua chanzo cha tatizo hilo pamoja na kufanya matengenezo ya mabehewa na maeneo ambayo yameharibika.

 

Baadhi ya abiria waliokuwa ndani ya Treni hiyo wanaeleza tukio hilo lilitokea ghafla na wengi wao walipatwa na mshituko ambapo walishukuru tatizo hilo kugundulika mapema na hatua kuchukuliwa.

 

Wamesema kwa kuwa wanaendelea na safari wanamuomba Mungu waweze kufika salama katika maeneo ambayo wao wanaelekea huku wakitoa wito kwa serikali kuendelea kuboresha miundombinu hiyo ya reli.

Post a Comment

0 Comments