UJENZI WA MADARAJA KUNUFAISHA WANANCHI






Na Mwajabu Hoza , Kigoma.
WANANCHI wa vijiji vya Nyamidaho, Bitale wilaya ya Kigoma Nyamihanga wilaya ya Buhigwe  wameanza kusafirisha mazao yao kupeleka katika masoko mbalimbali mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa madaraja matatu ya mawe yanayokadiriwa kuwa na dhamani ya zaidi ya milioni 300 ambayo yanaunganisha vijiji vyao na barabara kuu ya kuelekea Kigoma mjini.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa ziara ya wajumbe wa bodi ya mfuko wa barabara mkoani Kigoma yenye lengo la kukagua miundombinu ya barabara maeneo ya mjini na vijijini.

Nao Wakazi wa vijiji hivyo wanaeleza changamoto yao ya awali kabla ya kupata daraja kuwa walishindwa kusafirisha mazao ambayo wanalima kutokana na kukosekana kwa daraja la uhakika na hivyo kuishia kuuza mazao hayo kwenye masoko yaliyopo vijiji jirani.

Zuwena Gwilerula na Dani Mikidadi wanasema kutokana na Ukosefu wa daraja hulazimika kuzunguka Kijiji kimoja ili kufika katika Kijiji kingine na kutumia gharama kubwa za usafiri na usafirishaji lakini pia hata huduma muhimu za matibabu imekuwa ngumu kuyafikia kwa wakati.

Bosko Laiki naye anaeleza kuwa kumekuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao ikiwemo Mihogo, mahindi, maharage na mazao mengine lakini hawezi kuyafikisha sokoni kutokana na changamoto ya daraja na hivyo kufanya uchumi wao kuendelea kuzorota.

Aidha wameishukuru serikali kwa ujenzi wa madaraja hayo ambayo yamekuwa  chachu ya kusafirisha bidhaa zao pamoja na kupata huduma muhimu za kiafya lakini pia wakatumia fursa ya vyombo vya habari kuomba kufikishiwa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami ili kuondokana na changamoto ya barabara wakati wa kipindi cha masika.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA mkoa wa Kigoma Mhandisi Godwin Mpenzile akitoa maelezo kwa wajumbe wa bodi amesema madaraja matatu ambayo yamejengwa kwa teknolojia ya mawe yamegharimu Zaidi ya shilingi milioni 300 kwa ushirikiano wa serikali,and the only nguvu za wananchi na ufadhili wa ubelgiji kupitia shirika la ENABLE   ambalo lilikuwa likitekeleza mradi wa kilimo.

Akizungumzia ujenzi wa madaraja kwa Mkoa wa Kigoma  mhandisi Mpenzile amesema hadi Sasa wamejenga madaraja 110 ambayo yamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kumudu kufikia huduma za kimsingi wanazozihitaji maeneo mengine na hata kubadilisha hali ya kiuchumi kwa wananchi kutokana na mwingiliano mkubwa wa kibiashara.

Meneja TARURA makao makuu Hamidi Mataka amesema katika mwaka fedha 2023/2024 serikali inakusudia kujenga madaraja 180 kupitia teknolojia ya mawe yenye thamani ya shilingi bilioni 20 teknolojia ambayo itasaidia kupunguza gharama za ujenzi ambapo matumizi ya ujenzi wa madaraja hayo ungefikia milioni 40 hivyo serikali imeokoa kiasi cha milioni 20 kutokana na ujenzi huo wa madaraja ya mawe.

" Tumezoea ujenzi wa kawaida kuchukua kokoto ,nondo na vifaa vingine ambavyo hivyo vinaongeza gharama ya ujenzi lakini huu ubunifu wa ujenzi wa kutumia mawe unapunguza nusu ya gharama" alisema Mataka

Kaimu Mwenyekiti bodi ya mfuko wa barabara (RFB) Tanzania Octavian  Mshiu amesema ujenzi wa madaraja hayo ni ubunifu mkubwa ambao umewezesha wananchi 500 kupata ajira lakini pia madaraja hayo yatawezesha wananchi kumudu kufanya shughuli za uzalishaji mali kwa kusafirisha mazao yao.

"Hiki Kijiji cha Nyamihanga tangu Uhuru ama  kuumbwa kwa dunia hawajawahi kuona magari yakifika katika Kijiji chao lakini kukamilika kwa daraja hili la Malagalasi litasaidia wakulima kusafirisha mazao yao lakini pia kupata huduma za muhimu maeneo ya mjini kwa sababu Kijiji hiki kitaunganishwa na Kigoma mjini kimiundombinu " alisema 

 Mshiu amesema wao kama bodi wataendelea kutoa fedha kwa TARURA ili madaraja mengi Zaidi yaendelee kujengwa ambapo Kati ya madaraja 180 ya mawe  yanayojengwa nchi nzima madaraja 24 yatajengwa Mkoani Kigoma katika wilaya zote za Mkoa.

 

Post a Comment

0 Comments