WATENDAJI WA KATA WATAKIWA KUCHAPA KAZI



Na Mwajabu Hoza, Kigoma.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma kupitia mapato yake ya ndani imetoa pikipiki 14 zenye dhamani ya shilingi milioni 45 kwa ajili ya watendaji wa kata ili kuwarahisishia utendaji kazi kwa ufanisi katika maeneo yao.

Pikipiki ambazo zimegawiwa  kwa watendaji wa kata ni hatua ya ukamilishaji wa shughuli za mwenge wa uhuru kitaifa ambao ulibakiza zoezi la ugawaji wa pikipiki kwa watendaji katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Akikabidhi pikipiki hizo pamoja na kadi kwa niaba ya kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa 2023 mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli amesema pikipiki hizo ziwe chachu ya kuongeza uwajibikaji na utendaji kazi kwa ufanisi na sio zitumike kwa maslahi ya watu binafsi kujiingizia kipato.

"Rais Samia Suluhu Hassan anatujali katika kurahisisha ufanyaji kazi, kilichobaki ni KUCHAPA KAZI na hivi ni vifaa vya kutusaidia na kama leo hii Mtendaji wa kata atastaafu ama kuhama hii pikipiki itaendelea kuwepo kwenye kata yako itatumika na waliopo,  itunzwe isitumike kuwa mtaji wa mtu kwa maana ya kuwa daladala ama bodaboda hapana, mara leo ipo Buhigwe hapana   itumike kama ilivyokusudiwa " amesema  Salim Kalli.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Mwantumu  Mgonja  amesema pikipiki hizo zitawasaidia watendaji wa kata kurahisisha shughuli mbalimbali ikiwemo  mchakato wa ukusanyaji wa mapato, kufuatilia miradi ya maendeleo na  kuwafuata wananchi kusikiliza kero zao.

"Hapa ni ndani ya Manispaa ni Imani yangu wataongeza ufanisi wa kiutendaji" amesema.

Baadhi ya watendaji akiwemo Ramadhani Kalukula na Mwavita Rusovu wametoa shukran zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasana,  uongozi wa Mkoa, Wilaya na ofisi ya Mkurugenzi kwa kuwafikiria wao na kuwapatia vyombo vya usafiri ambapo wameelezwa kuwa kuna baadhi ya kata ni kubwa na ilikuwa changamoto kwao kuzifikia kwa wakati  hivyo pikipiki hizo zitarahisisha utendaji kazi wao na kuahidi kuzitunza.

Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma ujiji inakata 19 na pikipiki hizo zimetolewa kwa kata 14 huku kata moja ilikuwa imeshapatiwa pikipiki kwa awamu ya kwanza na hivyo  bado kata nne ambazo zimeelezwa kuingizwa katika bajeti ili kutimiza pikipiki 19 katika kata zote.

Post a Comment

0 Comments