PROF. NOMBO ATETA NA WAKUU WA VYUO VYA UALIMU VYA UMMA JUU YA MAGEUZI YA ELIMU




Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam
Serikali imesema Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 Toleo la 2023 na Mabadiliko ya Mitaala yamefanyiwa kazi kwa muda mrefu ili kumfikia kila mdau katika kutoa maoni.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo Jijini Dar es Salaam Oktoba 30, 2023 alipokutana na Wakuu wa Vyuo vya Ualimu vya Umma ambapo amesema kuwa katika kuhakikisha hilo njia mbalimbali za kushirikisha wadau ikiwemo mitandao ya kijamii, vyombo vya habari, barua pepe na mijadala zimetumika kuwafikia wadau.

Prof. Nombo amesema kuwa hata katika mijadala mikubwa ya makundi mbalimbali mawazo  yaliwasilishwa kupitia viongozi wa makundi na kufanyiwa kazi katika kuhakikisha kuwa kila maoni yaliyotolewa yanafika katika kamati husika.

Katibu Mkuu huyo amesema mkakati wa utekelezaji wa mageuzi hayo utaanza kidogo kidogo ambapo utachukua miaka kumi kukamilisha, hivyo amewataka Wakuu hao kujiandaa kuanza utekelezaji huo.

Aidha, amewataka Wakuu hao kufuata sheria, taratibu, kanuni  na miongozo mbalimbali ya serikali wakati wa kutekeleza majukumu yao pamoja na kutumia vizuri nguvu kazi na vifaa ili kuviwezesha vyuo kuweza kujitegemea.

Naibu Katibu Mkuu Dkt. Franklin Rwezimula amewataka wakuu hao kutekeleza miongozo ya serikali pale inapotolewa na kama kuna changamoto wizara ipo tayari kutatua changamoyo hizo ili kurahisisha utekelezaji majukumu yao.

Dkt. Rwezamula amesema ili kuondoa changamoto mbalimbali zinazohusu matumizi ya fedha, wizara itawajengea uwezo wakuu hao katika maeneo ya namna maandalizi ya  bejeti,  utunzaji wa taarifa za mapato na matumizi ya fedha na masuala ya manunuzi.

Mkuu wa Chuo cha Ualimu Marangu Corinel Chambulila amemshukuru Katibu Mkuu kwa kuwafafanulia vyema juu ya mageuzi ya elimu yanayotarajiwa kufanyika hivi karibuni pamoja na kuomba Wizara kuendelea kutoa miongozo ambayo itawasaidia kutekeleza majukumu yao.

Post a Comment

0 Comments