UTPC KUZINDUA RASMI KAMPENI YA KITAIFA YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA


Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) unatarajia kuzindua rasmi kampeni ya kitaifa ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia hapo kesho tarehe 25 Novemba 2023 mkoani Morogoro.

Hayo yamebainishwa na Afisa Programu, Utawala na Maendeleo ya Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania, Hilda Kileo akizungumza katika siku ya pili ya mafunzo ya usawa wa kijinsia wanayopatiwa jumla ya waandishi 28 kutoka katika Klabu zote nchini. 

Amesema kuwa kampeni hiyo itahitimishwa katika kilele chake tarehe 10 Disemba 2023 ambapo itakwenda sambamba na Mkutano Mkuu wa UTPC kwa mwaka 2023  utakaofanyika jijini Dodoma. 

Ameongeza kuwa kampeni hiyo itafanyika kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii, ikiwa na lengo la kuibua mijadala itakayosaidia kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa ukatili wa kijinsia nchini.

Aidha, Klabu zote 28 za Waandishi wa Habari zilizo nchi nzima zitashiriki kikamilifu katika kampeni hii ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Kauli mbiu ya kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa mwaka huu wa 2023 ni "WEKEZA ZUIA UKATILI WA KIJINSIA".

Post a Comment

0 Comments