WAANDISHI WA HABARI WEKENI MASLAHI YA UMMA MBELE, MNAPOTEKELEZA WAJIBU WENU WA KITAALUMA.


Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Waandishi wa habari wametakiwa kuweka maslahi ya umma mbele wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kitaaluma ya kuandika habari.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya usawa wa kijinsia mkoani Morogoro. 

Ameongeza kuwa, waandishi wanapaswa kuwa mabalozi wazuri katika kuandika masuala ya usawa ya kijinsia na kujiamini kuwa wana nguvu na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kwani tasnia ya habari ni muhimili wa nne wa taifa usio rasmi.

"Ni vema waandishi wa habari mkaweka maslahi ya umma mbele wakati unapoandika stori, kamwe usikubali mtu anapokukwamisha au kukukataza kuandika kuhusu maslahi ya Taifa, kumbuka sisi hatuwajibiki kwa watawala, tunawajibika kwa umma".

Naye Afisa Programu, Utawala na Maendeleo ya Klabu, Hilda Kileo amesema lengo kuu la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari namna ya kuandika habari zitakazowezesha kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu kwa watanzania wote wakiwemo  wanawake na wasichana kama ilivyoainishwa katika lengo namba 5 la SDGs pamoja na kuhakikisha mipango ya maendeleo ya Tanzania na SDGs zote zinatekelezwa kwa kizingatia usawa wa kijinsia. 

Jumla ya Waandishi 28 kutoka katika Klabu zote za Waandishi wa Habari nchini wamefaidika na mafunzo haya ambayo yamefadhiliwa na ubalozi wa Sweden.

Mafunzo haya yameanza leo Novemba 23-25, 2023 mkoani Morogoro na hii ikiwa  ni awamu ya pili sasa. Awamu ya kwanza ya mafunzo yalifanyika Agosti 7-8, 2023.



Post a Comment

0 Comments