WATOTO 505,840 KUPATIWA KINGATIBA KIGOMA


Na Mwandishi Wetu, Kigoma.
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OR -TAMISEMI inaendesha zoezi la umezeshaji  vidonge vya kingatiba kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya Minyoo ya Tumbo na Kichocho kwa watoto kuanzia miaka mitano hadi 14 katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi ikiwemo mkoa wa Kigoma. 

Akitoa Taarifa kwa Umma kuhusu  zoezi hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Katibu Tawala  Mkoa wa Kigoma Albert Msovela amesema mkoa umepokea vidonge 793,000 aina ya Plaziquantel na 548,200 Albendazole kwa lengo la kuchanja watoto 505,840 walioko ndani na nje ya utaratibu wa shule. 

Amesema Wizara Afya kupitia mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele, imedhamiria kutekeleza mpango huo ili kuhakikisha watanzania wanakuwa na Afya bora kwa kuwakinga dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika. 

Amesisitiza kuwa ili malengo ya serikali yaweze kufikiwa, jamii inapaswa kutoa ushirikiano kwa wataalam wa Afya katika kuwatambua walengwa na kuhakikisha wanafikiwa kisha  kupatiwa huduma. 

"Nitoe wito kwa wadau wa Afya na jamii kwa ujumla kuhakikisha tunashirikiana na serikali katika utekelezaji wa zoezi hili ili walengwa wote waweze kufikiwa, aidha jamii iendelee kukumbuka wajibu wake katika kuhakikisha watoto wanapata chanjo mbalimbali kuendana na miongozo ya Sekta ya Afya" amesisitiza Msovela. 

Akitoa Taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa zoezi hilo Mratibu wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele Mkoa wa Kigoma Innocent Msilikale, amesema utekelezaji wa zoezi hilo umekuwa ukikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo uelewa duni wa wananchi kuhusu umuhimu wa zoezi hilo pamoja na hofu itokanayo  na uwepo wa maudhi madogo madogo yanayosababishwa na matumizi ya dawa hizo. 

Aidha amesema katika kukabiliana na changamoto hizo wanaendelea kutoa elimu kwa wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kingatiba, namna bora ya kukabiliana na maradhi ya tumbo  sambamba na kuhamasisha ulaji shuleni wakati wa utoaji dawa.

Zoezi la ugawaji kinga tiba ya magonjwa ya minyoo ya tumbo na Kichocho  linatekelezwa kuanzia tarehe 13 hadi 25 Novemba 2023, likihusisha Halmashauri Nane za Mkoa wa Kigoma.

Post a Comment

0 Comments