KILIMO CHA UYOGA KUWANUFAISHA WANANCHI KASULU - KIGOMA







Na Mwandishi Wetu, Kasulu - Kigoma
Utafiti uliofanyika katika Wilaya ya Kasulu  mkoani Kigoma umebaini kilimo cha zao la Uyoga kitawanufaisha wananchi wa eneo husika kwakuwa uhitaji wake ni mkubwa katika soko. 

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mkufunzi Mwandamizi wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Halima Kazindolo kwenye warsha ya wadau kuhusu tathimini ya mradi wa uzalishaji  wa Uyoga katika wilaya hiyo. 

Amesema kabla ya kuanza utekelezaji wa kilimo hicho ni lazima hamasa itolewe kwa wakulima kuwa kuna uhakika wa soko pamoja na kuchukua muda mfupi  hadi kukamilika kwake.

Naye Andrew Ching’ole kutoka  Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) amesema kuwa kupitia tathimini hiyo amejifunza Uyoga unalimika kipindi chote cha mwaka na kukamilika ndani ya miezi miwili kabla ya kufika sokoni.

Meneja wa SIDO Mkoa wa Kigoma, Gervas Ntahamba amebainisha kuwa utafiti huo umefanyika katika vijiji vinne katika wilaya hiyo na kutoka na taarifa ambayo haijakamilika hivyo kupitia uwasilishaji huo watapata maoni na mawazo kwa ajili ya maboresho.

Awali akifungua uwasilishaji huo  mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu, Audax Kamugisha  amewataka washiriki kuusikiliza kwa makini ili kubaini kama umefikia malengo yaliyokusudiwa.

“Kilimo cha Uyoga ni kikubwa na chenye manufaa kwa jamii kwenye kuwaingizia pesa ila kama hujaelezwa huwezi kujua undani wake lakini tukiielewa tathimini wenzetu waliofanya tunaweza kuingia katika kilimo hiki vizuri,”amesema.

Post a Comment

0 Comments