RC KIGOMA AONGOZA MDAHALO KUELEKEA KILELE MIAKA 62 YA UHURU






Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Kuelekea Kilele cha Maadhimisho  ya Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Mkoa wa Kigoma umeendesha Mdahalo uliolenga kuangazia na kubainisha mafanikio ambayo Mkoa pamoja na Taifa kwa Ujumla limeyapata tangu nchi ilipopata Uhuru. 

Akifungua mdahalo huo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema hatua za kimaendeleo zilizofikiwa tangu nchi kupata Uhuru ni jambo la kujivunia na inapaswa kuwa chachu katika kuzidi kusimamia vizuri miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita. 

Amesema ni muhimu kwa watanzania kutafakari na kufahamu mustakabali wa Taifa kwa lengo la  kufahamu kuhusu  hali halisi ya maendeleo kabla na baada ya kupata Uhuru ili  kujiwekea mipango endelevu ya kitaifa. 

Akichangia mdahalo huo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Lebba amesema wakati nchi inapata Uhuru mkoa ulikuwa na watoa huduma za Afya chini ya mia moja ambapo kwa sasa waliopo kazini ni 2332 huku vituo vya kutolea huduma za Afya vilikuwa chini ya Kumi ambapo kwa sasa  vipo 307.

Ameendelea kueleza kupitia mdahalo huo kuwa, Mkoa umewezeshwa kutoa huduma  za X ray, uchunguzi wa Figo na kuongezeka kwa utolewaji wa Huduma nyingine  za kibingwa kadhalika katika kufanikiwa  kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi vya UKIMWI kutoka  Asilimia 2.9 hadi 1.7. 

Upande wake mwakilisha mada kwa niaba ya Afisa Elimu Mkoa wa Kigoma, Mwalimu Shukurani Kalegamye amesema wakati nchi inapata Uhuru mkoa ulikuwa na shule mbili za Sekondari na Shule za msingi 73 ambapo mpaka kufikia mwaka 2023 mkoa una jumla ya Shule za Sekondari 237 na za msingi 722. 

Naye Katibu wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma  Sayi Samba amesema mafanikio makubwa yameendelea kuonekana ikiwa ni pamoja na uboreshwaji wa miondombinu, kuimarishwa kwa biashara na masoko pamoja na kuimarika kwa ushirikiano wa kimataifa.

Post a Comment

0 Comments