SERIKALI MKOANI KIGOMA YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA WAFANYABIASHARA WADOGO





Na Mwandishi Wetu, Kigoma.
Serikali mkoani Kigoma imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Samia Suluhu kwa kushirikiana na wafanyabiashara wadogo maarufu wamachinga ili kuimarisha uchumi wa kundi hilo. 

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ametoa kauli hiyo alipokutana na uongozi  wa Shirikisho la Umoja wa Wamachinga Mkoa wa Kigoma(SHIUMA)  na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto na kuimarisha Mazingira ya utendaji kazi kwa kundi hilo kwa kuwa linayagusa maisha ya watu wengi. 

Amesema  kupitia kikao hicho, wamekubaliana kuimarisha muunganiko kati ya wafanyabiashara wadogo na Taasisi za kifedha ili kuwawezesha kupata mitaji, maeneo sahihi ya kufanyia biashara pamoja na kujiimarisha kiuchumi wao binafsi. 

"Nisingependa kuona wafanyabiashara wadogo wanabaki katika hali hiyo muda wote bali  iwe ni daraja la kufikia kuwa wafanyabiashara wakubwa na hata kuwa wawekezaji wenye mitaji mikubwa" amesisitiza Andengenye. 

Upande wake Katibu wa SHIUMA Mkoa wa Kigoma Ali Mvano amesema malengo ya kikao hicho yalikuwa ni kumfahamisha Mkuu wa Mkoa  kuhusu , majukumu ya shirikisho, kujadili pamoja na kupokea maelekezo na ushauri kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili. 

Aidha Mvano ametoa wito kwa wajasiriamali wanaofanya shughuli zao nje ya shirikisho hilo kujiunga ili kupata usimamizi wa  haki zao pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria  na taratibu za nchi. 

Pia ametoa wito kwa wajasiriamali wote mkoani hapa kushiriki zoezi la kujisajili katika kanzi data ili waweze kutambuliwa na kuipa urahisi serikali katika kuwafikia na kuwapatia  huduma mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments