WAHITIMU WA UHASIBU WATAKIWA KUITUMIKIA JAMII KWA UADILIFUI









Na Mwandishi Wetu, Kigoma.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengeye amewataka wahitimu wa chuo cha Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kampasi ya Kigoma, kuwa waadilifu na wazalendo katika kazi zao wanapoenda kuitumikia jamii .

Hayo ameyazungumza Mkuu wa wilaya ya Kigoma, Salum Kalli kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kigoma, katika mahafali ya 21  ya chuo hicho na ya  kwanza kwa kampasi ya Kigoma.

Amesema, kuwa mzalendo na muadilifu kutaweza kusaidia kuboresha huduma katika jamii ukizingatia kada hiyo kuwa muhimu na kutegemewa na jamii na taifa kwa ujumla.

Aidha Mh Kalli amesema serikali inatambua mchango wa chuo cha TIA ambao umekuwa ukitolewa na chuo hicho kwa kutoa wataalamu katika sekta mbalimbali za uzalishaji na kutoa mchango muhimu kwenye jamii na Taifa kwa ujumla.

Amesema  serikali inakiangalia chuo hicho kwa karibu sana ndio maana imekijumuisha  katika mradi unaofadhiliwa na serikali ya Tanzania katika ujenzi wa chuo hicho mjini Kigoma  kampasi ya  Kigoma unaogharimu kiasi cha zaidi ya  shilingi bilioni 11 bambapo kwa sasa umefikia asilimia 26 ya ujenzi wake.

“Mradi huo ni fursa kwa jamii inayozunguka katika eneo la ujenzi wa chuo hicho ikiwemo kupata ajira rasmi na zisizo rasmi na kuweza kukuza kipato chao kwa mtu mmoja mmoja na mkoa wa ujumla,”amesema Kalli.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha TIA, Profesa William Pallangyo amesema katika tawi la Kigoma jumla ya wanafunzi 910 wamehitimu huku idadi ya wahitimu wote wa chuo cha TIA kwa mwaka 2022/23 ni 13,218  kwa Dar, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Kigoma na Singida.

“Hatua ya kusheherekea mahafali ya kwanza kwa mkoa wa Kigoma ni mafanikio makubwa kwetu, kwa kupiga hatua katika eneo la uendeshaji wa  mafunzo, tafiti, ushauri wa kitaalamu na miundombinu ya kusomea,”amesema Pallangyo.

Amesema mahafali hayo yameenda sambamba na kutambulisha masomo mapya ya ngazi ya shahada katika uhasibu,ugavi na ununuzi, usimamizi wa biashara na uongozi wa rasilimali watu  zitakazotolewa chuoni hapo.

Ameongeza kuwa, hatua hiyo ya kuwa na masomo hayo ngazi ya shahada  itawapa fursa wadau mbalimbali wa ndani ya Tanzania na nchi jirani kujiendeleza kielimu baada ya kusogezewa huduma hiyo karibu.

"TIA Kigoma imeendelea kuwajengea wanachuo msingi wa mahiri na kuwapa elimu ya nadharia na vitendo hivyo kuwawezesha kuajiriwa na kujiajiri pindi watakapohitimu masomo yao.

"Pia TIA kigoma imeendelea kutoa ushauri wa kitaalamu katika maeneo ya usimamizi wa biashara, masoko, usimamizi wa rasilimali watu, ununuzi na ugavi, taaluma ya uhasibu na fedha kwa wafanyabiashara wa mkoani Kigoma kupitia washauri wataalamu wa ndani" amesisitiza Mkuu huyo wa Chuo.
 
Nae Mwenyekiti wa bodi ya TIA, Said Musendo  amewasihi  wahitimu hao kwenda kuzitumia taaluma zao vizuri na kuwaletea matunda na bila kusahau kujiendeleza kielemu kwasababu elimu haina mwisho na hapo ni mwanzo wa elimu yao hivyo bado wanasafari ndefu ya elimu.

Baadhi ya wahitimu wa chuo hicho wamesema wataenda kutumia elimu yao waliyopata darasani kujikwamua kiuchumi na kujiajiri kwani ni moja ya masomo waliyokuwa wakifundishwa wakati wakiwa chuoni.
 

Post a Comment

0 Comments