ZAIDI YA 100% YA WENYE VVU WATAMBUA HALI ZAO KIGOMA





Na Mwandishi Wetu, Kigoma.
Asilimia  119.4 ya wanaoishi na Virusi vya UKIMWI mkoani Kigoma wanatambua hali zao huku wakiendelea kudumisha ufuasi wa dawa na ili kufubaza makali ya  VVU. 

Mkuu wa wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Masala amesema hayo  alipomuwakilisha  Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwenye hafla ya Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo kimkoa  imefanyika katika Kijiji cha Songambele wilayani Buhigwe.

Amesema katika kukabiliana na maradhi hayo, Serikali  imefanikiwa  
kuanzisha vituo 93 kwa ajili ya  kutoa tiba na mafunzo kwa wanaoishi na VVU ikiwa ni sawa na Asilimia 97.9 ya mahitaji halisi ya mkoa. 

Sambamba na mafanikio hayo, Kanali Masala ameitaka jamii mkoani hapa  kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya tatizo kuongezeka uzito uliopitiliza pamoja na kujenga tabia ya kupima Afya mara kwa mara hali itakayosaidia kubaini maradhi katika hatua za awali ikiwemo ugonjwa wa  kisukari na shinikizo la damu. 

Mkuu huyo wa wilaya amesema  Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu, imedhamiria kuyatumia maadhimisho  hayo kwa lengo la kutoa elimu, hamasa  pamoja na kushirikiana na Asasi za kiraia ili  kuhakikisha huduma za VVU na UKIMWI zinayafikia makundi mbalimbali kwenye Jamii. 

Akitoa taarifa ya hali ya utekelezaji wa Afua mbalimbali za UKIMWI kimkoa, Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Kigoma Innocent Msilikale  amesema kuanzia Januari hadi Oktoba 2023,  jumla ya watu 409,785 wamepima VVU na kati yao 4105 kugundulika na maambukizi ya UKIMWI ikiwa ni sawa na Asilimia 0.93 ya waliopima. 

Aidha Katika kukabiliana na VVU, Mkoa umeendelea kuhakikisha huduma za upimaji wa VVU zinapatikana wakati wote,  kutoa tohara kwa wanaume wenye umri wa miaka 15 na kuendelea, kutoa dawa kinga, kusajili wateja wenye VVU na kutoa mafunzo kwa watoa huduma za Afya ili kuwajengea uwezo katika kutoa elimu kwa jamii. 

Aidha Msilikale amezitaja changamoto zinazoendelea kukinzana na utekelezaji wa Afua mbalimbali za UKIMWI kuwa ni baadhi ya wateja kuacha matumizi ya dawa  na kujihusisha na tiba mbadala jambo linalosababisha kuzorota kwa Afya zao na hata kusababisha vifo.

Post a Comment

0 Comments