UFAULU WA UPIMAJI WA KITAIFA KIDATO CHA NNE, DARASA LA NNE WAONGEZEKA.






Na Mwandishi Wetu, Dodoma 
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) leo Januari 07, 2024 limetangaza matokeo ya Mtihani Upimaji wa Kitaifa Kidato cha Pili, ambapo Jumla ya Wanafunzi 592,741 kati ya 694,769 wamefaulu sawa na asilimia 85.31. Kiwango hicho cha ufaulu kimeongezeka kwa asilimia 0.13 ikilinganishwa na asilimia 85.18 ya Wanafunzi waliofaulu Mtihani huo mwaka jana.

Akitangaza matokeo hayo Katibu Mtendaji wa NECTA Dkt. Said Mohamed amesema Jumla ya Wanafunzi 759,799 walisajiliwa kufanya Mtihani huo, wakiwemo Wasichana 405,878 na wavulana 353,921

 Kati ya Wanafunzi waliofaulu kuendelea na Kidato cha Tatu Wasichana ni 314,949 sawa na asilimia 83.66 na wavulana ni 277,792 sawa na asilimia 87.28.

Kwa upande wa matokea ya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne amesema Jumla ya Wanafunzi 1,287,934 kati  ya 1,545,330 sawa na asilimia 83.34 wamefaulu kwa kupata madaraja ya A, B, C na D.

Dkt. Mohamed amesema kumekuwa na ongezeko la ufaulu kwa asilimia 0.39 kwa Wanafunzi wanaoendelea na darasa la Tano ikilinganishwa na mwaka 2022.

Kati ya Wanafunzi hao Wasichana ni 681, 259 sawa na asilimia 84.79 na wavulana ni 606,675 sawa na asilimia 81.78.

Katibu Mtendaji huyo amebainisha Baraza la Mitihani limefuta matokeo yote ya Wanafunzi 178 waliofanya udanganyifu na Wanafunzi 3 walioandika lugha isiyo na staha  katika Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne. 

Pia limewafutia matokeo Wanafunzi 28 waliofanya udanganyifu na Wanafunzi 14 walioandika lugha isiyo na staha katika Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili.


Post a Comment

0 Comments