WARATIBU WA SERIKALI WILAYANI KASULU WAMETAKIWA KUHAKIKISHA MAENEO WANAYOSIMAMIA YANAKUWA MASAFI





Na Mwandishi Wetu, Kasulu Kigoma.
Ili kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu waratibu wa shughuli mbalimbali za kiserikali wilayani Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuhakisha maeneo wanayoyasimamia yanakuwa katika hali ya usafi  ikiwemo takataka kuondolewa kwa wakati sehemu zinapohifadhiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu ameyabainisha hayo hivi karibuni kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC).

 Kikao kilichokuwa na lengo la kuibua vyanzo vipya vya mapato ili vipate kujumuishwa kwenye bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

“Kasulu ama Mkoa wa Kigoma tumepakana na mikoa yenye viashiria vya ugonjwa wa Kipindupindu na ugonjwa huu wote tunatambua unasababishwa na uchafu, sasa Kasulu inakuwa na uzalishaji wa taka umekuwa mkubwa tusipokuwa makini kuzidhibiti tutaingia kwenye matatizo ya Kipindupindu” amebainisha.

Aidha, Mwakisu aliwataka watendaji wa kata kuhakikisha watoto wanaandikishwa kujiunga na elimu ya msingi pamoja na ile ya sekondari.
 
Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu, Eliya Kagoma aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuja na kauli mbiu ya kupambana na vitendo vya ramli chonganishi maarufu kama Kamchape.
 
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya hiyo, Mbelwa Chidebwe alishauri kuwepo na usimamizi mzuri wa shughuli za ukusanyaji wa mapato ili malengo yaliyowekwa na halmashauri yaweze kutimia kwa mwaka huo wa fedha.

Post a Comment

0 Comments