WASIOJULIKANA WAIBA MITA ZA MAJI KIGOMA UJIJI





Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WIZI wa mita za maji umetokea katika maeneo mbalimbali ya manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo watu wasiojulikana wamedaiwa kuiba mita hizo kwenye nyumba za watu.

Mmoja wa waathirika wa vitendo hivyo vya wizi, Elius Lukwala mkazi wa Nazareth Sokoni Manispaa ya Kigoma Ujiji ameiambia blog hii kwamba umetokea wizi wa mita ya maji nyumbani kwake mwanzoni mwa wiki hii mida ya saa nane usiku baada ya kusikia maji yakimwagika.

Amesema kuwa baada ya kutokea wizi huo ameripoti tukio hilo katika kituo kikuu cha polisi mjini Kigoma sambamba na kuripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya majii safi na maji taka Kigoma Ujiji (KUWASA) kwa ajiili ya kupatiwa mita mpya.
 
Hata hivyo amesema kuwa ameshangazwa na KUWASA kuwataka wateja kulipa shilingi 100,000 kwa ajiili ya kupatiwa mita nyingine wakati mwathirika huyo siyo aliyesababisha mita kuibwa huku mamlaka ikikataa mita kufungwa ndani ya uzio wa nyumba husika.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA,Mhandisi Poas Kilangi amethitisha kutokea kwa wizi wa mita za maji na kulitaja eneo la Nazareth kama moja ya maeneo yaliyoathirika na wizi huo ambapo hadi sasa wana taarifa ya mita 15 kuibwa kwenye nyumba mbalimbali.
 
Kilangi amesema kuwa wamesharipoti matukio hayo polisi na Mkuu wa polisi wilaya ya Kigoma na timu yake ya upelelezi wanaendelea kuchunguza matukio ya wizi huo ili kubaini hasa sababu za mita hizo kubwa ikiwemo kujua zinapelekwa wapi na kufanyia nini.
 
Akizungumza kitendo cha watendaji wa mamlaka hiyo kukataa mita kufungwa ndani ya uzio Kilangi amekiri ni muongozo wa mamlaka na hiyo inazuia usumbufu ambao wasoma mita wanaupata na kubainisha kuwa mita kukaa nje siyo tatizo na kwamba suala la kuangalia kwa nini zinaibwa akikiri pia wateja kutozwa shilingi 100,000 waweze kuwekewa mita nyingine.

Post a Comment

0 Comments